Vyombo vya usalama nchini Misri na Cyprus vimebaini kuwa mtu aliyeiteka nyara ndege ya shirika la ndege la EgyptAir baada ya kumrubuni rubani kuwa anavilipuzi kiunoni mwake, hakuwa gaidi bali alikuwa na matatizo ya kisaikolojia.

Mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Seif Eldin Mustafa aliilazimisha ndege hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Alexandria kwenda Cairo, kubadili muelekeo na kwenda nchini Cyprus ambapo alijisalimisha kwa vyombo vya usalama.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus, Loannis Kasoulides alieleza kuwa huenda matatizo ya kisaikolojia ya mtu huyo yana uhusiano mkubwa na suala la uhusiano wa kimapenzi na mkewe wa zamani.

Alisema kuwa mtu huyo aliilazimisha ndege hiyo kubadili muelekeo na kutua Cyprus ambapo yupo mkewe huyo wa zamani, na baada ya kutua tu alitoa masharti ya kuletewa mkewe huyo wa zamani katika uwanja huo wa ndege ili azungumze naye, masharti ambayo Polisi iliyatimiza.

Baadae Mustafa alijisalimisha kwa vyombo vya usalama akitoka kwenye ndege hiyo akiwa ameweka mikono juu.

Mapema leo, Polisi nchini humo wamemfikisha mahakamani Mustafa akituhumiwa kwa makosa mbalimbali kutokana na kitendo chake cha kuteka ndege. Kadhalika, Jeshi la Polisi nchini humo limesema linaendelea kuwahoji ndugu zake.

 

Mwanasiasa Kuwania Nafasi ya Urais ZFA
Watu 7 Wauawa Ajali ya Ndege Canada