Afisa Mtendaji Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Barbara Gonzalez, ametuma salamu Young Africans kwa kuwaambia wajiandae kupigika kwa Mkapa kesho Jumamosi (Julai 03).

Simba SC itakuwa mwenyeji wa Young Africans kwenye mchezo huo, ambao ulipaswa kuchezwa Mei 08 lakini uliahirishwa kufuatia mkanganyiko wa muda uliokuwa umepangwa na Bodi ya Ligi (TPLB).

Barbara amesema Simba SC imejiandaa kila idara kuelekea mchezo huo, na wana matumaini makubwa ya kushinda na kutwaa ubingwa kwa mara ya nne mfululizo.

“Tupo tayari kwa mchezo, tumejiandaa katika kila idara, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutashinda na kutwaa ubingwa kupitia kwa watani.”

“Tunatarajia kushinda, tunataka kushinda kila mchezo na kila kombe, hivyo mchezo wetu wa nusu fainali ya ASFC dhidi ya Azam FC ulikuwa kama kupasha misuli joto kwa DABI hii, hivyo wapinzani wetu wajiandae kupata AIBU, tumepania kubeba kila kitu.”

Barbara jana Alhamis jioni alishuhudia mazoezi ya kikosi cha Simba, Uwanja wa Mo Simba Arena akiambatana na viongozi wengine wa klabu hiyo.

Simba SC inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 73, inahitaji alama tatu kujihakikishia ubingwa msimu huu.

Young Africans yenye alama 67, inashika nafasi ya pili kwenye msimamo, inatakiwa kushinda mchezo wa kesho Jumamosi ili kuendeleza Presha ya ubingwa msimu huu dhidi ya Mabingwa Watetezi Simba SC.

Timu hizo kongwe zimesalia kwenye mbio za ubingwa, kufuatia Azam FC kufikisha alama 64 huku ikisaliwa na michezo miwili mkononi.

EndapoAzam FC itashinda michezo yake dhidi Simba SC na Ruvu Shooting, itafikisha alama 70 ambazo hazitawatosha kufanikisha kuwa mabingwa msimu huu.

Simba SC, Young Africans zaonywa
Chadema wakaidi agizo la Rais Samia, wadai ‘hawatapiga goti’