Mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, Bilionea Saniniu Laizer ameikabidhi Serikali shule mpya ya msingi aliyoijenga kwa gharama ya Shilingi Milioni 466.8 kwenye Kitongoji cha Namelock, Kijiji cha Naepo, Kata ya Naisinyai wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Akisoma risala wakati wa kukabidhi shule hiyo mwanafamilia wa Laizer, Simon Siria amesema shule hiyo itawanufaisha wanafunzi wa jamii ya wakulima na wafugaji na ina madarasa saba.

Siria amesema shule hiyo ilianza kujengwa darasa moja na wananchi wa
kitongoji cha Namelock na kijiji cha Naepo mwaka 2017 ndipo bilionea Laizer akaimaliza mwaka huu.

Amesema walilazimika kujenga shule kutokana na adha walizokuwa wanapata wanafunzi hao wakati wa mvua wanafunzi kwani huwa wanashindwa kuvuka korongo kwenda shule ya msingi Naepo iliyopo kilomita 1.5 kutoka katika eneo hilo.

“Shule hii itakuwa mkombozi kwa wanafunzi wa eneo hili kwani wengine ni wadogo na iliwalazimu kutembea kilomita 2.5 kwenda shule ya msingi Naisinyai na wengine kwenda Naepo,” amesema Siria.

Akizungumza wakati akikabidhi shule hiyo kwa Serikali Bilionea Laizer amesema imemgharimu jumla ya Sh. Milioni 466.8 na hadi hivi sasa kuna wanafunzi 30 wanaosoma hapo.

Shule hiyo ina madarasa saba, matundu 10 ya vyoo na nyumba mbili za walimu watakaoweza kuishi familia nne.

“Tunaomba serikali itupatie walimu na pia tunaomba shule hii iwe ya mchepuo wa kiingereza ili wanafunzi watakaosoma hapo wawe bora kwenye taaluma yao,” amesema Bilionea Laizer.

Trump: Rais wa kwanza wa Marekani kushtakiwa mara mbili
Onyango ampigia 'SALUTI' kocha Matola