Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku amewanyooshea kidole wanasiasa wote wa zama hizi nchini kwa ubabaishaji kuhusu kanuni ya miiko ya uongozi ya kutenga biashara na siasa.

Akizungumza jana wakati akiwasilisha mada katika kongamano la kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere lililofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichoko jijini Dar es Salaam, Mzee Butiku alisema kuwa wakati wa TANU, Mwalimu na viongozi wengine waliweka miiko ya uongozi na kwamba moja kati ya kanuni zake ilikuwa kutenga biashara na siasa.

Alisema katika kanuni hiyo ya uongozi, kiongozi alitakiwa kuwa mkulima au mfanyakazi  ambaye hashiriki katika shughuli zozote za kibepari. Mzee Butiku aliongeza kuwa kiongozi alipaswa kuchagua kuwatumikia wananchi au kujikita katika kusaka utajiri.

“Katika siasa za hivi sasa wanasiasa wote wamekuwa wanajitahidi sana kukataa kanuni hii na wamekuwa wakibabaisha,” alisema Mzee Butiku. ”Msibabaishe,” alisisitiza.

Mjadala wa kutenga siasa na biashara katika zama hizi umekuwa kizungumkuti kwani wanasiasa wengi wamewekeza katika biashara mbalimbali kwa lengo la kujiongezea kipato.

Mdahalo huo ulioongozwa na Spika wa Bunge la Kumi, Anne Makinda ulihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa zamani ambao walitoa nasaha zao kuhusu busara za Mwalimu na mwenendo wa kisiasa nchini.

Makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula aliyewasilisha mada katika mdahalo huo, alisema kuwa chama chake kinachoshikilia dola kimekuwa kikizingatia maadili ya uongozi ikiwa ni pamoja na jitihada za kupambana na rushwa.

Mangula aliwaonya makada wa chama hicho ambao wameanza kutoa zawadi na misaada kwa lengo la kutengeneza mazingira ya kuchaguliwa katika uchaguzi ujao na kueleza kuwa katika awamu hii hilo halitawezekana.

DC Mtaturu Afanya Kongamano Kumuenzi Baba wa Taifa
TBS waangushiwa 'tofali’ kashfa ya kuvushwa kontena 100 bandarini