Aliyekua nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba amempachika jina Cristiano Ronaldo na kumuita “real leader”.

Drogba ametangaza jina hilo la utani kwa Ronaldo alipokua akihojiwa na kituo cha televisheni cha klabu ya Real Madrid (Madrid TV) kuhusu shujaa huyo wa The Meringues pamoja na timu ya taifa ya Ureno.

Drogba, amesema mshambuliaji huyo anapaswa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia ‘Ballon d’Or’ kwa mwaka 2016 kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa kwa upande wa klabu na timu yake ya taifa, ambazo zote kwa pamoja ameziwezesha kutwaa ubingwa wa barani Ulaya.

“Nimecheza dhidi ya Ronaldo kwenye fainali ya UEFA mwaka 2008 ambapo Man United walishinda,

“Ni kiongozi halisi na anastahili kushinda tuzo ya Ballon d’Or kutokana na kiwango bora alichokionesha Real Madrid na Ureno. Licha kwamba kwenye fainali ya Euro dhidi ya Ufaransa alitoka mapema, lakini mchango wake ulichangia kuwapa taji Ureno.” Drogba aliiambia Madrid TV.

Ronaldo ambaye ni mshindi wa tuzo ‘Ballon d’Or’ mara tatu, anapewa nafasi kubwa ya kuchukua kwa mara nyingine tena, tofauti na washindani wengine ambao watatajwa na shirikisho la soka duniani baadae mwaka huu.

Mshindani mkubwa wa Ronaldo katika tuzo hiyo kwa miaka ya hivi karibuni Lionel Messi, tayari anaonekana kushindwa kufuatia mafanikio hafifu aliyoyapata kwa msimu wa 2015-16, ambapo aliisaidia klabu yake ya FC Barcelona kutwaa ubingwa wa La Liga pekee huku akichemka kwa upande wa timu ya taifa lake la Argentina, ambayo ilishindwa kutwaa ubingwa wa Copa America licha ya kutinga katika hatua ya fainali ya michuano hiyo.

Wachezaji wengine wanaotarajiwa kumpa changamoto kubwa Ronaldo ni Luis Suarez na Neymar waote wa FC Barcelona pamoja na mshambuliaji wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa Antoine Griezmann.

Ronaldo tayari ameshatajwa katika orodha ya wanaowania tuzo ya mchezo bora wa mwaka barani Ulaya kwa msimu wa 2015/16 akiwa sambamba na Gareth Bale (Real Madrid na Wales), Gianluigi Buffon (Juventus na Italia), Antoine Griezmann (Atlético Madrid na Ufaransa), Toni Kroos (Real Madrid na Ujerumani), Lionel Messi (Barcelona na Argentina), Thomas Müller (Bayern München na Ujerumani), Manuel Neuer (Bayern München na Ujerumani), Pepe (Real Madrid na Ureno) pamoja na Luis Suárez (Barcelona na Uruguay).

Video: Dude - Tunaiomba Serikali isiwe nguvu ya soda
Claudio Ranieri: Riyad Mahrez Haendi Popote