Aliyekua kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Emmanuel Amunike amesema uongozi wa klabu ya El-Makkasa, ulibadilisha nafasi yake kutoka kocha mkuu na kuwa mkurugenzi wa vituo vya kukuza na kulea vijana barani Afrika.

Uongozi wa El-Makkasa ulimtangaza Amunike kushia nafasi ya kocha mkuu Februari 02, baada ya mkataba wa mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Misri Ahmed Hossam ‘Mido’ kufikia kikomo.

Taarifa iliyotolewa jana jumapili na uongozi wa klabu hiyo, ilieleza nafasi ya kocha mkuu kwa sasa inashikwa na Ehab Galal, baada ya kumkabidhi Amunike cheo kingine.

“Bado mimi ni sehemu ya klabu, sijafukuzwa kazi kama ilivyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari, ninatarajia kupambana vilivyo katika nafasi yangu mpya ili kuiletea mafaniio klabu ya El-Makkasa,” amesema Amunike.

“Wakati nikifanya kazi Tanzania, viongozi wa El-Makkasa walikuja Dar es salaam, tukazungumza nao mambo kadha wa kadha, pia walizungumza na serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuwekeza katika soka husasan kujenga vituo vya kulea na kukuza soka kwa vijana. Huu maradi umelenga kuanzishwa kwenye nchi za Tanzania, Mali na ikiwezekana Nigeria kwa kuanzia.”

“Tulijadili sana suala la kuwekeza katika hivi vituo, ninaamini kwa uzoefu wangu katika soka la Afrika, kuna matunda mazuri yatapatikana kupitia vijana watakaokuzwa na kulelewa kwenye vituo hivi ambavyo vitakua chini ya klabu ya El-Mekkasa.”

Kwa sasa klabu ya El-Mekkasa inaendelea kupambana katika harakati za kujinusuru kushuka daraja, ikiwa nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi ya Misri, huku ikimiliki alama 14.

Amunike alibahatika kuiongoza El-Makkasa kwenye mchezo dhidi ya  Smouha na Al Entag Al Harbi ambayo ilimalizaika kwa sare ya bao moja kwa moja, na baadae alipoteza dhidi ya Tala’ea El Gaish kwa kufungwa bao moja kwa sifuri kwenye mchezo wa kombe la Misri (Egyptian Cup).

Amunike anaendelea kukumbukwa na wadau wa soka nchini, kufuatia kuiwezesha Taifa Stars kufuzu fainali za AFCON 2019, zoezi ambalo lilishindikana tangu mwaka 1980.

Video: CCM yajuta kumtosa Membe, Mbowe azidi kuwasha moto
Jaffar Iddy ang'oka Azam FC