Shirikisho la soka duniani FIFA limeionya Mexico, kufuatia vitendo vilivyoonyeshwa na mashabiki wao, wakati wa mchezo wa kwanza wa kundi A uliowakutanisha na Ureno kwenye fainali za kombe la mabara zinazoendelea nchini Urusi.

FIFA wamelitahadharisha shirikisho la soka la Mexico, kwa kulitaka liwafikishie ujumbe baadhi ya mashabiki, ambao walidiriki kumtukana mwamuzi wa mchezo wao dhidi ya Ureno ambao ulimalizika kwa sare ya mabao mawili kwa mawili.

Mashabiki wa Mexico walifikia hatua ya kumtusi mwamuzi, kufuatia kitendo cha kusimamisha mpira kwa lengo la kupata maelekezo ya maafisa wanaoendesha mfumo wa Video, ambao unatumika kutoa maamuzi ya mwisho kwenye michuano ya kombe la mabara.

Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya FIFA, Anin Yeboah, ameliambia shirikisho la soka nchini Mexico “Kuna kikundi cha mashabiki wenu kimeonyesha utovu wa nidhamu wakati wa mchezo wa kwanza dhidi ya Ureno, tunawaomba mkikanye kisirudie tena tabia hiyo chafu, kama tabia hiyo itajirudia tena, hatutosita kuchukua hatua za kinidhamu dhidi yenu”

FIFA imewahi kuiadhibu Mexico kwa kosa la mashabiki wao kubeba mabango yenye ujumbe wa kuunga mkono ushoga, wakati wa fainali michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018.

Hatua hiyo ilitoa msukumo kwa wachezaji wa Mexico kuunda umoja ambao unapinga vitendo hivyo vya mashabiki wakati wanapokua katika majukumu ya kuishangilia timu yao.

Leo Mexico itacheza dhidi ya New Zealand katika mji wa Sochi, ukiwa ni mchezo wao wa pili hatua ya makundi.

Majimaji FC Yajivua Gamba, Yatema 16
Muigizaji maarufu wa Afrika Kusini Apigwa Risasi