Mradi wa barabara ya njia sita kutoka Kimara hadi eneo la Maili Moja jijini Dar es Salaam, utahusisha ujenzi wa madaraja makubwa pamoja na barabara moja ya juu (flyover).

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Babarabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale amebainisha hayo alipokuwa akikagua mradi huo unaogharimu Sh140 bilioni, ukitarajiwa kukamilika Januari 2020.

Amesema kuwa barabara ya juu itajengwa katika eneo la Mloganzila, hivyo kuongeza idadi ya barabara za juu baada ya ile ya njia panda ya Tazara.

Mfugale ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Estim Construction, chini ya usimamizi wa Tanroads.

“Hii barabara itakuwa na urefu wa Kilometa 19.2, na baada ya kukamilika barabara hii itakuwa na uwezo wa kupitisha magari 8,000 kwa kila barabara kwa siku,” alisema na kuongeza kuwa hivi sasa magari takribani 50,000 yanayopita yanasababisha msongamamo mkubwa.

Amefafanua kuwa hadi sasa ujenzi wa mradi huo unaotumia fedha za ndani umefikia asilimia 5.8. Zaidi ya nyumba 2000 zilivunjwa ili kupisha utekelezaji wa mradi huo.

Serikali imeendelea kufanya juhudi za kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, ambapo mbali na ujenzi wa barabara ya juu ya Tazara (Mfugale Flyover), daraja la Kigamboni pamoja na mpango huo wa Mlonganzila, maeneo mengine yanayotajwa ni pamoja na njia panda ya Ubungo, Kamata na Morocco.

Flyovers saba ziko kwenye mpango wa kujengwa katika mpango wa awamu ya kwanza ya kukabiliana na msongamano wa magari jijini humo.

Prof. Mbarawa azindua mradi mkubwa wa maji
Walinzi waliomsaidia Mo Dewji wafunguka