Kiungo mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzana Bara Simba SC Perfect Chikwende anaamini ushiriki wa klabu yake mpya kwenye michuano mingi kwa msimu, itamsaidia kuendeleza makali dimbani, kama ilivyokua Zimbabwe.

Chikwende alikamilisha usajili wa kujiunga na Simba SC mwishoni mwa juma lililopita, akitokea FC Platinum ya nchini kwao Zimbabwe, baada ya kuonesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Mshambuliaji huyo amesema anaamini usajili wake ndani ya klabu ya Simba SC utakua na mantiki kubwa, na ushiriki wa klabu hiyo kwenye michuano mingi kwa msimu itaweza kumsaidia.

Amesema anatambua Simba SC inahitaji mchango wake katika kufikia lengo la kutetea ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho (ASFC), hivyo hana njia mbadala zaidi ya kuboresha kiwango chake kila kukicha, ili aendeleze makali kama alivyokua kwenye michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Simba SC.

Chikwende amejiunga na Simba SC akitokea kwenye kikosi cha FC Platinum ya Zimbabwe baada ya kuonyesha uwezo mkubwa kwenye michezo miwili ya mzunguuko wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

“Nipo tayari kutumika kuisaidia Simba, nafurahi kuwepo hapa na najua nitapata nafasi kubwa ya kukuza kiwango changu maradufu kutokana na ukweli kwamba Simba inashiriki michuano mingi hivyo ni nafasi kwangu kucheza mara kwa mara.” Amesema Chikwende.

Licha ya kuifungia FC Platinum bao moja kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya Simba SC mjini Harare, Chikwende alishindwa kufurukuta kwenye mchezo wa mkondo wa pili uliochezwa Dar es salaam mapema mwezi huu.

Hata hivyo kiwango kilichooneshwa na mshambuliaji huyo, ndio kilikua kichocheo kikubwa kwa viongozi wa Simba SC kumsajili kupitia dirisha dogo lililofungwa rasmi Januari 15.

Simba SC iliiondosha FC Platinum kwa jumla ya mabao manne kwa moja na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa BArani Afrika, ambapo wamepangwa kundi A dhidi ya Al Ahly ya Misri, AS Vita ya DR Congo pamoja na El Mereikh ya Sudan.

Biden aanza kwa kutengua sera za Trump
Majaliwa avalia njuga uzalishaji mkonge