Nahodha wa wawakilishi wa Zanzibar kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika, JKU, Ponsian Maliki amewahahakishia wazanzibari kuwa, wana kila sababu ya kulipiza kisasi licha ya kufungwa mabao manne kwa sifuri dhidi ya Sports Club Villa ya nchini Uganda katika mchezo wa mkondo wa kwanza.

Ponsian, alitoa uhakika huo, baada ya kikosi cha maafande wa jeshi la kujenga uchumi visiwani Zanzibar (JKU) kuwasili mjini Unguja kikitokea mjini Kampala.

Amesema kilichotokea nchini Uganda mwishoni mwa juma lililopita, ilikua kama bahati mbaya kwao, lakini wamebaini udhaifu wa wawapinzani wao ambao watakuja nchini kupambana nao siku ya ijumaa kwenye uwanja wa Amaan.

“Ni kweli tulifungwa 4-0 kule Uganda lakini tunamatumaini ya kushinda mchezo wa marejeano, ni kweli 4-0 ni mengi lakini tutapigana kiume tuwafunge hawawezi kutufunga nje ndani, naamini kama washambuliaji wetu watatumia nafasi watakazozipata tutukomboa mabao 4-0 na tutaengeza”.

Amesema kwa sasa wameingia kambini kwenye hoteli ya Island View, iliopo Kilimani mjini Unguja, na kocha wao Malale Khamsini atayafanyia kazi mapungufu yaliyopelekea kupoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Sports Club Villa.

Klabu ya JKU baada ya kupokea kichapo hicho cha bao 4-0 kutoka kwa SC Villa na Ijumaa itaikaribisha klabu hiyo uwanja wa Amaan mjini Zanzibar na ili JKU ifanikiwe kusonga mbele inahitaji ushindi wa bao 5-0.

Emmanuel Petit: Arsene Wenger Anapaswa Kuondoka
Mbinu Tano Zitakazoipa Ushindi Arsenal Mbele Ya Barca