Nahodha na Mshambuliaji wa Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC John Bocco, amesema akili za wachezaji zinafikiria mchezo wa kwanza wa kurejea kwa ligi dhidi ya Maafande wa Ruvu Shooting utakaopigwa siku ya Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es salaam.

Bocco amesema wanajua ligi ikirejea itakuwa ngumu kutokana na maandalizi ya timu nyingine lakini wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri wakianza na mchezo wa kwanza siku ya Jumapili.

Bocco ameongeza kuwa wachezaji wote wako katika hali nzuri morali ipo juu huku wakiendelea kupokea mafunzo kutoka kwa makocha wao.

“Tunajua ligi itakuwa ngumu timu zote zimejiandaa lakini nasi tunaendelea vizuri na kwa sasa akili zetu ziko katika mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Ruvu lengo letu likiwa ni kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wetu,” amesema Bocco.

Bocco amesema wanapata mafunzo bora kutoka kwa makocha hali inayowafanya kuendelea kuwa bora kama walivyofanya juzi walipocheza mechi mbili za kirafiki siku moja na kushinda mabao saba.

“Makocha wetu wanafanya kazi kubwa kutufanya tuwe bora na matarajio yetu ni kuhakikisha tunatetea ubingwa na kufanya vizuri kwenye michuano ya FA,” alimalizia Bocco.

Waziri Mpango aishukuru IMF kuisamehe Tanzania deni la Bilioni 33
Msamaha wa Magufuli kwa zimamoto watoka na onyo kali