Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kuichunguza Halmashauri ya Manispaa ya Temeke baada ya Mbunge wa jimbo hilo kusema manispaa hiyo inadaiwa na Benki ya CRDB.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Februari 26, 2021 akiitaka taasisi hiyo kuchunguza kubaini iwapo kuna ufisadi uliofanyika kwenye madai ya Manispaa hiyo kuchukua mkopo Benki ya CRDB ambapo serikali haikuhusishwa katika suala hilo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Majengo ya Ofisi na Madarasa pamoja na Bweni la Wanafunzi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini, Dar es salaam, Mbunge wa jimbo la Temeke, Dorothy Kilave alimuomba Rais Magufuli Serikali Kuu iweze kuisaidia Manispaa ya Temeke kulipa deni la shilingi Bilioni 12.195 ambalo Manispaa hiyo inadaiwa na Benki ya CRDB.

Mbunge huyo ameeleza kuwa Manispaa ya Temeke ilichukua mkopo wa shilingi Bilioni 19 kutoka CRDB kwa ajili ya kulipa mafao ya wale ambao maeneo yao yalitakiwa kubomolewa ili kujenga miradi ya DMDP, mkopo ambao kwa sasa unalipwa kwa awamu, kwa manispaa hiyo kuilipa benki ya CRDB shilingi Bilioni 4.8 kwa mwaka.

“Mbunge wa Temeke naye anataka Serikali ikalipe deni kwa mkopo ambao Serikali haikuhusika, mambo ya ajabu, Manispaa mmekaa mkaongea na CRDB mazungumzo hayajulikani, inawezekana ni ya kificho, mmeshindwa kulipa mnataka Serikali ikalipe deni, hilo msahau, mtalibeba wenyewe” amesema Rais Magufuli.

“Kwani shule zote zilizojengwa Tanzania na wote waliojenga Mahospitali walienda kukopa CRDB?, kwanza ni kukosa nidhamu ya fedha za Serikali kwenda kuzi-involve kwenda kukopa kwenye Commercial Bank halafu mnakwenda kulipia fidia,” ameongeza rais Magufuli.

Katibu Mkuu EAC kuchaguliwa kesho Februari 27
Waziri Simbachawene apewa siku saba