Kiungo Mshambuliaji wa Namungo FC Shiza Ramadhan Kichuya amesema hajawahi kuchukia wala kushangaa, kuona Mashabiki wa Young Africans wakimzomea kila anapocheza dhidi ya timu yao.

Kichuya aliendelea kukutana na kadhia hiyo juzi Jumamosi (Februari 04), wakati wa mchezo wa Mzunguuko wa 22 wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulimalizika kwa Namungo FC kukubali kufungwa 2-0.

Kichuya ambaye aliwahi kuifunga Young Africans katika michezo mitatu tofauti akiwa na Simba SC, amesema kitendo cha kuzomewa na Mashabiki wa Young Afrika anakipokea kama chachu ya kuendelea kupambana na kufanya vizuri anapokuwa uwanjani.

“Mashabiki wa Young Africans waendelee kunizomea, tena ninawaomba wanizomee zaidi kwa sababu hiyo kwangu inaniongezea nguvu ya kupambana.”

“Halafu hiyo inanionesha kuwa wanakubali na wanatambua mimi ni mtu gani. Kama wangekuwa hawanizomei maana yake mimi sio lolote.”

“Kwa hiyo waendelee kunizoea, mimi hata sichukii wala siumizwi na hilo.” amesema Kichuya

Tangu alipojiunga na Namungo FC misimu mitatu iliyopita Kichuya hajawahi kuifunga Young Africans, licha ya kupata bahati ya kuwa kwenye kikosi cha klabu hiyo mara zote.

600 wajitokeza huduma ya uzazi pandikizi
Zaidi ya 500 wafariki kwa tetemeko la ardhi