Bodi ya wakurugenzi ya Barcelona hii leo itakutana kujadili namna ya kumuenzi gwiji wao, Johan Cruyff, aliyefariki dunia juma lililopita.

Kwa mujibu wa gazeti la michezo la kila siku (Katalunya Sport), imeelezwa kwamba dhamira ya kikao hicho ni kuubadili jina Uwanja wa Nou Camp na kuupa jina la gwiji huyo wa Uholanzi ambaye enzi za uhai wake alifanya kazi kama mchezaji na kocha.

Cruyff aliyefariki dunia Alhamisi baada ya kusumbuliwa na maradhi ya saratani ya mapafu akiwa na umri wa miaka 68, ameshinda mataji ya La Liga na Copa del Rey uwanjani hapo akiwa na Barca, kabla ya kutwaa mataji mengine kibao akiwa kocha likiwemo Kombe la Ulaya mwaka 1992.

Barcelona inatafakari namna ya kumpa heshima ya kudumu Cruyff kutokana na mchango wake mkubwa kwa klabu hiyo enzi za uhai wake.

Mtoto wa kiume wa Cruyff, Jordi, ambaye kama baba yake amechezea Barca na Uholanzi, alikutana na makamu wa rais wa klabu, Jordi Cardoner kuanza kujadili mpango huo.

Uholanzi Nao Waamua

Viongozi wa chama cha soka Uholanzi (KNVB) kimetangaza kwamba wataubadilisha jina uwanja wa Amsterdam Arena na kuuita Johan Cruyff ili kumpa heshima yake mshindi huyo wa tuzo tatu za Ballon d’Or aliyefariki kwa ugonjwa wa saratani ya mapafu.

Rais wa KNVB, Michael van Praag, amesema: “Siwezi kuchelewa kuubadilisha jina Uwanja wetu na kuwa Johan Cruyff Arena. Ni heshima kubwa tunaweza kumpa gwiji huyu”.

Super D: Tujenge MGM Grand Garden Arena Ya Tanzania
Mbowe awataja watakaokula matunda ya Kazi ya Lowassa Chadema