Magari kadhaa ya mizigo yamechomwa moto katika Jimbo la Kwa Zulu Natal, baada ya maelfu ya waandamanaji wanaotaka kuachiwa kwa Rais wa Zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, kuingia mitaani na kuchoma magari kadhaa katika Jimbo hilo, ikiwa ni hatua ya kuishinikiza serikali kumuachia kiongozi huyo wa zamani.

Msemaji wa Kikosi cha Ukaguzi na Usalama Barabarani katika Jimbo hilo, Zinhle Mngomezulu, amesema magari kadhaa ya mizigo, magari ya mafuta yamechomwa moto na waandamanaji kuanzia usiku wa Ijumaa na Jumamosi asubuhi, na kusababisha hali ya taharuki katika jimbo hilo.

Katika video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, magari mbalimbali yanaonekana yakiwa yanateketea kwa moto huku waandamaji wakikimbia huku na kule, wakiimba nyimbo na kubeba mabango yanayoshinikiza kuachiwa kwa Zuma.

Hata hivyo Jeshi la polisi nchini Afrika Kusini, limesema mpaka sasa limewakamata watu takribani 27 kwa kosa la kuandamana na kusababisha vurugu katika Jimbo la Kwa Zulu Natal, ambapo Msemaji wa Polisi, Jay Naicker amesema jeshi la polisi linaendelea kukabiliana na maandamano hayo lililoyaita haramu na yanayovunja sheria.

Wakati hayo yakiendelea, Taasisi ya Jacob Zuma Foundation imesema ina wasiwasi mkubwa kutokana na kufungwa kwa Zuma kwa sababu ya hali yake ya kiafya, hasa katika kipindi hiki ambacho kuna mlipuko wa ugonjwa wa Corona.

Polisi Tanzania FC: Gerald Mdamu anaendelea vizuri
Azam FC yairarua Trans Camp