Leo ilikuwa siku ambayo Rais John Magufuli ametoa uamuzi mzito wa kubadilisha nafasi za uongozi wa ngazi ya juu zaidi kwa viongozi ambao amefanya nao kazi, baada ya kumuondoa Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa katibu Mkuu Kiongozi, akiwa mstari wa mbele kutangaza wanaotumbuliwa majipu.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli uliotangazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu kwa maneno machache, umezua maswali mengi kwa wananchi na wafuatiliaji wa siasa hususan mstari unaoeleza kuwa ‘atapangiwa kazi nyingine’.

“Kufuatia uteuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue atapangiwa kazi nyingine,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu.

Mstari huo umeonekana kupigiwa mstari mkuu na kuongeza maswali kuwa kuna kila dalili kuwa Rais Magufuli ‘amemtumbua jipu’ kimyakimya Balozi Ombeni Sefue.

Uteuzi huo umeendelea kukuna vichwa vya wadau, kwakuwa siku sita zilizopita, gazeti la ‘Dira ya Mtanzania’ liliandika habari mbili ambazo zilielezea kile lilichokiita ‘uchafu’ wa Kiongozi huyo mkubwa.

Habari hizo zilikuwa na vichwa vya habari ‘Uchagu wa Ombeni Sefue Ikulu’ pamoja na ‘Magufuli anaishi na Jipu Ikulu’ iliyoendelezwa katika safu ya pili huku ikiwaahidi wasomaji kuwa ingeendelea toleo la leo (Machi 7).

Gazeti hilo lilieleza mambo mengi lililodai yamefanywa na Balozi Sefue, ikiwa ni pamoja na kuingiza maslahi yake binafsi kwenye michakato ya zabuni za Ujenzi wa daraja la Kinondoni, ujenzi wa chuo kikuu cha Dodoma na mingine. Pia lilimhusisha na kusimamia na kushinikiza Uteuzi wa Mkurugenzi wa Bohari la Dawa Tanzania (MSD) waliyedai hana utaalam wowote wa dawa bali ni msomi wa masuala ya jamii (Sociology).
Hata hivyo, Serikali ilikanusha vikali taarifa hizo na kulitaka Gazeti hilo kuomba radhi kwa ‘upotoshaji na uzushi’ vinginevyo hatua kazi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Hali hiyo imeacha vitendawili kichwani kwa wengi kwa kuunganisha picha na matokeo wanayoyaona ili kupata taswira sahihi ya nini hasa sababu ya uteuzi huo unaomuweka kando Balozi Sefue kwamba atapangiwa kazi nyingi. Kwanini hawezi kusubirishwa hadi hiyo kazi ngingine ijulikane..? Hapo ndipo jamaa wa maskani wanapokuna vichwa na kuanza tena kubishana kuhusu ‘kutumbuliwa jipu’ au la.

Hata hivyo, muda mfupi kabla ya kutangaza uamuzi huo, Rais Magufuli alisifu kazi nzuri na kubwa aliyoifanya Balozi Sefue kwa zaidi ya miezi mitatu aliyokaa naye Ikulu.

Lakini, inawezekana Rais amechukua uamuzi wake alioupanga tangu muda mrefu na anaona kuna sehemu Balozi Sefue ataenda kufanya kazi vizuri zaidi kwa maslahi mapana ya Taifa.

 

Madiwani wauwakia mradi unaohamasisha 'Ushoga' Shinyanga
Magufuli amuondoa Balozi Ombeni Sefue, ateua Katibu Kiongozi Mpya