Wakati wakurugenzi watatu wa wakala wa majengo Tanzania (TBA), wakisimamishwa kazi na Waziri mkuu Kasim Majaliwa mtendaji mkuu wa wakala huo Arch. Daud Kondoro ametakiwa kujitathmini kuhusu utendaji wake kutokana na kusuasua kwa miradi mbalimbali waliyopewa na Serikali.

Waziri Mkuu amewasimamisha kazi wakurugenzi hao hii leo Novemba 18, 2019 wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa ofisi ya Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) unaofanyika katika eneo la Njedengwa lililopo jijini Dodoma.

Wakurugenzi hao waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa idara ya ujenzi, Arch. Humphrey Killo, Kaimu meneja wa miradi, Abdallah Awadh na Kaimu mkurugenzi idara ya ushauri Arch. Hamis Kileo.

Waziri Mkuu amesema amechukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa TBA katika miradi mbalimbali waliyopewa na Serikali likiwemo jengo la NEC ambalo ujenzi wake ulianza julai, 2017 na kutakiwa kukamilika juni 2018.

Hata hivyo mradi huo bado haujakamilika na ujenzi wake umesimama licha ya uwepo wa fedha za Serikali shilingi bilioni 13 za kukamilisha mradi huo ambapo Waziri Mkuu amehoji sababu za mradi huo kutokamilika kwa wakati kitu ambacho hakileti taswira chanya.

“Watu wa TBA wana shida na hatuwezi kuwaacha na ni wazi sasa TBA wasipewe miradi kwa sababu hawawajibiki na wanadhani kwa kuwa ni taasisi ya Serikali ndio wataachwa wafanye mambo ya hovyo hii haikubaliki ni lazima kuwajibika na ninamtaka mtendaji mkuu wa wakala kujitathmini,” amefafanua Majaliwa.

Akijibu swali la Waziri Mkuu Kaimu Mkurugenzi wa idara ya ujenzi Arch. Humphrey Killo amesema jengo hilo limeshindwa kukamilika kwa wakati kwani walipokuwa wanaanza kazi walibaini kuwa kuna vitu vilisahaulika wakati wa uandaaji wa Bill of Quantities yaani (BOQ).

Amesema japo TBA ndio waandaaji wa ramani ya jengo na ndio wajenzi lakini bajeti ya awali ilikuwa sh. bilioni 10 wakati wa uandaaji wa michoro ya ujenzi gharama ziliongezeka na kufikia shilingi bilioni 13 walizokubaliana katika mkataba.

“Lakini wakati tunaendelea na kazi tuligundua kuna vitu vimesahaulika kwenye BOQ jambo lililoongeza bajeti ya ujenzi na kufikia shilingi bilioni 32 na ndio maana kuna uchelewaji wa ukamilifu wa mradi huu.” amefafanua Arch. Killo.

Kufuatia jibu hilo Waziri Mkuu amehoji endapo waliweka makubaliano na mwenye jengo juu ya ongezeko hilo la kutoka shilingi bilioni 13 hadi kufikia shilingi bilioni 32 na kudai kuwa hapo awali muhusika alipatana nao kiasi cha shilingi bilioni 10 kitu ambacho kwasasa kinachanganya.

Hata hivyo Arch. Killo ametoa sababu za kuongezeka kwa gharama za ujenzi huo kwa madai ya kugundua tofauti wakati wakiwa kwenye eneo la ujenzi kwamba kuna kazi zilitakiwa zifanyike lakini katika mkataba hazipo na kukiri kuwa hawakuwasiliana na muhusika.

“Miongoni mwa vitu vilivyosahaulika katika BOQ ya mradi huo ni pamoja na kutokuwepo kwa ghorofa ya nne katika jengo moja wanalolijenga ambalo ni la ghorofa nane, pia hapakuwa na paa la jengo la kuhifadhia vifaa mbalimbali vya tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC),” amebainisha Arch. Killo.

Waziri Mkuu Kasim Majaliwa akasema miradi mingi inayojengwa na TBA katika maeneo mbalimbali imeshindwa kukamilika kwa wakati na kumwagiza Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu, sera, bunge, kazi, vijana, ajira na walemavu Jenista Mhagama asitishe mkataba huo wa ujenzi na atafutwe mkandarasi mwingine.

Aidha amefafanua kuwa jengo la TAMISEMI lililopo katika mji wa Serikali limejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7 na kuwashangaa wataalamu hao huku akihoji iwapo kuna sababu za kuendelea kuwaacha ndani ya taasisi hiyo.

“TBA mmekiwa hamfanyi kazi vizuri wakuu wa mikoa na wilaya wanalalamika majengo hayakamiliki ni Serikali gani itakayowavumilia, mmeshindwa kutambua majukumu yenu na serikali haitasita kuchukua hatua stahiki ya matendo ya namna hii hivyo mnasimama kazi na mtendaji mkuu ajitahmini,” amesema Majaliwa.

Hata hivyo Waziri Mkuu ameagiza mkandarasi atakayepatikana kumalizia ujenzi wa jengo hilo ahakikishe mradi wa ujenzi huo unakamilika katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa na lijengwe kwa kutumia mfumo wa force account.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Novemba 19, 2019
Wakulima wa zao la viazi Makete walilia soko la pamoja