“Na mimi naamini mtanikumbuka kwa mazuri na sio kwa mabaya. Kwa sababau nime-sacrifice (nimejitolea) maisha yangu kwa ajili ya Watanzania masikini. Kwahiyo, tusimame pamoja, tusibaguane kwa vyama, tusibaguane kwa ajili ya dini zetu, tusibaguane hata kwa makabila yetu. Sisi tuijenge Tanzania yetu.”

Hayo ni maneno mazito aliyowahi kuyasema, Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati wa uhai wake, alipokuwa akiwahutubiwa wananchi akiwa kwenye ziara ya kikazi. Ni Dkt. Magufuli ambaye kwa sasa ametangulia mbele ya haki akiwa na umri wa miaka 61. Rais Mzalendo aliyewahi kujipunguzia mshahara wake na kupokea robo ya kiwango kilichokuwa kimepangwa. Akapunguza maisha ya starehe ya vigogo na kutumia fedha hizo kuwaneemesha pia Wananchi waliokuwa wanaishi kwenye umasikini. Akalinda rasilimali za nchi, akafuta wizi wa mabeberu, wao wakamshangaa yeye akaendelea kuwanyoosha bila woga kwa maslahi ya Tanzania.

Usiku wa Machi 17, 2021, Tanzania ilipata mshtuko mkubwa baada ya kuisikia sauti ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan akitangaza kwa masikitiko kifo cha Rais huyu Mzalendo na mchapakazi hasa, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli.

Mama Samia aliliambia Taifa kuwa Mheshimiwa Rais alifariki kwa ugonjwa wa moyo akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena chini uangalizi wa madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Alizaliwa Oktoba 29, mwaka 1959 katika jiji cha Chato, wakati huo Tanzania ikifahamika kama Tanganyika. Alisoma na kumaliza elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Chato kuanzia 1967 hadi 1974. Mwaka 1975 alijiunga na elimu ya sekondari, akisoma kwa nyakati tofauti kwa kuhama katika Shule za Sekondari ya Seminari ya Katoke iliyoko Biharamulo (1975-1977) na baadaye Lake Sekondari kati ya Mwaka 1977-1978.

Mwaka 1978, Magufuli alijiunga na elimu ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Mkwawa na kuhitimu mwaka 1981. Mwaka huohuo (1981) alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Koleji ya Mkwawa akisoma Stashahada ya Elimu ya Sayansi, akichukua masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu.

Elimu ilikuwa kipaumbele kwake, aliendelea na safari ya elimu na kupata Shahada ya Elimu ya Sayansi, akijikita katika Kemia na Hisabati. Katika kipindi hicho, Magufuli alifanya kazi ya ualimu hadi mwaka 1989. Ilipofika mwaka huo, aliamua kuacha ualimu na kuajiriwa na Kampuni ya Nyanza Cooperative Union akifanya kazi kama mkemia hadi mwaka 1995, alipofanikiwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chato kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Magufuli hakuwahi kukata tamaa, alijaribu ubunge akakosa, akaendelea na mapambano hadi alipochaguliwa wakati sahihi ulipofika.

Katika kipindi cha kwanza cha ubunge wake, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa ambaye sasa ni marehemu, alimteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi. Baada ya kuchaguliwa kwa mara ya pili kuwa Mbunge wa Chato katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2000, aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, na hii ilitokana na uchapakazi wake.

Magufuli aliendelea kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Chato kwa awamu nyingine mwaka 2005, ambapo Januari 4, 2006 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Katika kipindi cha urais wa Mzee Kikwete, Magufuli alifanya kazi kama Waziri wa Uvuvi na Mifugo kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2010, na baadaye Waziri wa Ujenzi tena kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 alipotangaza nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliingia kwenye mchakato wa kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015, uliokuwa na upinzani mkali kuanzia ndani ya CCM ambacho ni chama tawala, hadi nje ya chama hicho. Magufuli hakuwa kati ya watu 10 waliokuwa ‘wanatajwatajwa’, na hakuwa kwenye kundi lolote kati ya makundi mazito yaliyokuwa yanachuana vikali hadi nje ya mchakato.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Idara ya Oganizesheni, Dk. Mohamed Seif Khatibu kushoto akimkabidhi fomu ya kuomba nafasi ya kuwania Urais, Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (Juni 5, 2015).

Dkt. Magufuli aliheshimu sana Katiba ya CCM na utaratibu wa kuwania urais. Alichukua fomu bila mbwembwe na bila kuwatangazia watu, akapita kimyakimya kusaka wadhamini bila kufanya mkutano wowote. Watu walimuita ‘mzee wa kimyakimya’. Hakuna aliyemuona akiwa mbele ya mchuano mkali uliokuwepo. Lakini mwisho, busara za viongozi wa CCM vilimuweka Dkt. Magufuli kuwa kati ya wagombea watatu waliopigiwa kura kumpata mgombea mmoja.

Katika kinyang’anyiro hicho cha fainali ya wagombea watatu, Dkt. Magufuli alichuana na Dkt. Asha-Rose Migiro ambaye aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Bi. Amina Salum Ali, aliyewahi kuwa Balozi wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa.

Dkt. Magufuli aliibuka mshindi, akiteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015. Mengi ya kisiasa yalitokea ndani ya muda mfupi, hususan kutokana na mvutano ulioibuka ndani ya CCM, na hivyo baadhi ya vigogo wa chama hicho wakahamia upande wa upinzani. Dkt. Magufuli alichaguliwa na chama chake akiwa na Mama Samia Suluhu Hassan kama mgombea Mwenza wa urais.

Ingawa kulikuwa na ushindani mkali kati ya Dkt. Magufuli na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyeungwa mkono na vyama vitano vya upinzani vilivyounda umoja maarufu kama Ukawa, Dkt. Magufuli alishinda katika uchaguzi huo kwa asilimia 58%. Aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Novemba 5, 2015 na kuwa Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano, na Makamu wa Rais akawa Mama Samia Suluhu Hassan.

Katika kipindi cha miaka mitano, Rais Magufuli alifanya mambo mengi makubwa akitekeleza miradi mikubwa kwa midogo yenye lengo la kuinua maisha ya kila mwananchi. Alifanikiwa kupambana na rushwa, ufisadi na kurejesha nidhamu ya kazi. Alipambana vikali na vita zilizokuwa zinaonekana ni nguvu na akazishinda kwelikweli, ikiwa ni pamoja na vita dhidi ya dawa za kulevya, vita dhidi ya ujangili wa wanyama pori na vita ya ufisadi. Kikubwa zaidi ilikuwa kubana matumizi ya Serikali na kutumia fedha hizo kufanya miradi ya maendeleo kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi.

Kwa kasi hiyo, mwaka 2019, Chuo Kikuu cha Dodoma kilimtunuku Shahada za Uzamivu (PhD) ya heshima kwa kukuza uchumi wa nchi.

Mwaka 2020, Rais Magufuli aliandika rekodi itakayobaki kwenye historia ya Watanzania katika kizazi hiki na vizazi vyote vijavyo, akifanikiwa kuifikisha Tanzania katika Uchumi wa Kati. Hatua hiyo kubwa ilikiwa ikiwa imewahi zaidi kwa miaka mitano ilivyokuwa inatarajiwa. Yaani, Tanzania ilikuwa ikikadiriwa kufika uchumi wa kati mwaka 2025.

Mwaka 2020, Rais Magufuli alishiriki tena mchakato wa uchaguzi, akiomba kuchaguliwa tena. Alichaguliwa kwa kishindo kizito, akipata ushindi wa Asilimia 84.

Miradi ya Kimkakati:  

Dkt. Magufuli amefanya makubwa na yanayoonekana. Amefanikisha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) yenye kilometa zaidi ya 300 kutoka Dar es Salaam kwenda jijini Dodoma, na ukiwa na mpango wa kuinganisha Dar es Salaam na Mwanza. Tayari SGR imefika kwa asilimia 98 mjini Morogoro. Tayari Mkandarasi mwingine ameshasaini mkataba wa kujenga SGR kutoka Mwanza- Isaka yenye urefu wa Kilometa 3,141.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipata maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania TRC) alipotembelea banda la kampuni hiyo akiwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Maadhimisho ya Awamu ya Nne ya Wiki ya Viwanda kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam. 

Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere wenye (JNHPP-MW2115) ambalo litaweka historia ya kumaliza tatizo la umeme nchini, na kupata umeme wa ziada wa kuziuzia nchi za jirani.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli imefanikiwa kuboresha huduma za afya, miundombinu ya barabara na makazi na mengine mengi.

Alikuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingi na bara la Afrika. Profesa Lumumba wa Kenya, aliitumia sera na mwenendo wa kazi wa Magufuli akiitaka Afrika kuiiga, akaandaa wasilisho linalofahamika kama ‘Magufulification of Africa’.

Tanzania inamlilia Jembe, muongoza njia na mwenye maono ya aina yake. Leo ametangulia lakini maono yake na kazi yake itadumu milele. Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani, Rais John Pombe Magufuli.

Kenya, EAC zatangaza siku 7 za maombolezo, Kenyatta amlilia Rais Magufuli
Tanzia: Rais John Pombe Magufuli afariki dunia, taifa lamlilia