Kocha msaidizi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho (ASFC) Simba SC, Selemani Matola, amekanusha uvumi wa kuwa mbioni kuajiriwa na klabu ya Azam FC, ambayo imeonyesha kuwa kwenye mipango ya kujizatiti ili kuwa na msimu mzuri (2020/21).

Matola amekua akihusishwa na taarifa za kutakiwa na matajiri hao wa Azam Complex Chamazi, kufuatia kuwa na uwezo mzuri wa kutoa ushauri kwenye benchi la ufundi, kama alivyofanya wakati wote wa msimu wa 2019/20, akisaidiana na kocha mkuu wa Simba SC, Sven Vandenbroeck.

Kocha huyo mzawa ambaye aliwahi kucheza Simba SC na baadae kutimkia Afrika Kusini kujiunga na Super Sports United,  amesema hakuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizo (Tetesi), na ataendelea kubali Simba SC.

“Tetesi hizo hazina ukweli wowote. Azam FC hawajawahi hata siku moja kunifuata kuzungumzia jambo hilo, na wala sijawahi kukaa nao meza moja kuongea nao, ila tu nimekuwa nikiyasikia kama ninyi vyombo vya habari mnavyoyasikia,” amesema Matola.

Alipoulizwa endapo Azam FC watamfuata na kumtaka ajiunge nao kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu, amesema hawezi kuongea kitu ambacho hakijafanyika wala kujitokeza.

“Siwezi kuongelea kitu ambacho bado hakijafanyika, endapo wakifika ndiyo tutakaa na kuongea kama kukubaliana au la, lakini kwa sasa hakuna kitu kama hicho kabisa,” amesema.

Matola alijiunga na Simba katikati ya msimu wa 2019/20 akitokea Polisi Tanzania kuchukuliwa nafasi ya Denis Kitambi ambaye alitimuliwa kazi yeye na Kocha Mkuu wa wakati huo, Patrick Aussems ambaye naye nafasi yake ilizibwa na Mbelgiji mwenzake, Sven Vandenbroeck.

Young Africans wamnasa David Richard
Sinema ya Morrison, Young Africans kumalizwa Agosti 10