Kiungo wa klabu ya Arsenal ya England Matteo Guendouzi, kwa mara ya kwanza amezungumzia hali ya maisha ya klabu hiyo tangu waliposajiliwa wakati wa majira ya kiangazi akitokea kwenye klabu ya Lorient ya nchini kwao Ufaransa.

Guendouzi mwenye umri wa miaka 19, amesema tangu alipotua kaskazini mwa jijini London amekua na mazingira mazuri, huku akifurahia uwepo wake ndani ya kikosi cha kwanza cha The Gunners, ambacho ameshakitumikia mara 15.

Amesema ushirikiano mkubwa uliopo kikosini ndio kichocheo kinachoendelea kumpa ujasiri wa kupambana wakati wote, huku akiamini mwishoni mwa msimu huu watafikia lengo linalokusudiwa.

Jarida la Foot Mercato limefanya mazungumzo maalum na kiungo huyo ambaye hakudhaniwa kama angeweza kuzoea kwa haraka ligi ya England, kutokana na umri mdogo alionao.

Alipoulizwa ni vipi anajihisi tangu alipotua Emirates Stadium alijibu: “Ninajihisi furaha, na nimekua na ushirikiano mzuri kutoka kwa wenzangu, ninaamini mambo yataendelea kuwa mazuri zaidi ya nilivyo sasa.”

“Ninaamini wengi walihisi huenda ningekua na wakati mgumu wa kucheza katika ligi mpya, lakini changamoto hiyo niliifahamu mapema, ndio maana nimefanikiwa kwa uharaka kuzoea mazingira ya soka la England.”

“Ninawashukuru wachezaji wenzangu kwa kazi kubwa tunayoifanya, hadi kufikia sasa tumecheza michezo 16 bila kupoteza, ninaamini hali hii imedhihirisha ukomavu wa kikosi cha Arsenal, nina uhakika tutaendelea hivi hadi mwishoni mwa msimu huu.”

“Suala la kupata matokeo ya sare katika mchezo yetu mitatu iliyopita, nimelipokea kama changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi na meneja sambamba na wachezaji wote wa Arsenal, ninahisi tutakaporejea mwishoni mwa juma hili, mambo yatakua tofauti na tutarejea kwenye njia ya ushindi.” Alisema kiungo huyo kutoka Ufaransa.

Mwishoni mwa juma hili Arsenal watacheza mchezo wa mzunguuko wa 13 wa ligi kuu ya England, kwa kuikabili AFC Bournemouth watakaokua nyumbani kwenye uwanja wa Dean Court.

Usajili wa Guendouzi unatajwa kuwa sababu kubwa ya kuuzwa kwa aliyekua kiungo wa kutumainiwa klabuni hapo Jack Wilshere, ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya West Ham Utd.

Florentino Perez kumsajili Pedrinho
Claudio Ranieri achimba mkwara England

Comments

comments