Klabu ya Mbeya City imetamba kuwa itasajili mchezaji yoyote yule mzawa kutoka klabu za Simba na Young Africans lakini inaweza kuwanyang’anya wachezaji inayowahitaji kutokana na fungu la maana la usajili walilonalo kwa sasa.

Katibu mkuu wa klabu hiyo, Emmanuel Kimbe amesema kuwa baada ya kutofanya vema msimu uliomalizika kiasi cha kusubiri dakika za mwisho, kwa sasa wameona waanze mapema kuitengeneza timu yao kwa msimu ujao, na tayari wana fungu la pesa za usajili.

“Tumejifunza kutokana na makosa, hatutosubiri tena aibu hii iliyotufika msimu uliomalizika wa kusubiri dakika za mwisho na mechi za mwisho za Ligi Kuu ndiyo tubaki, ndiyo maana tumejiandaa mapema, tayari tuna fungu la kutosha, tunasubiri tu ripoti ya mwalimu atuambie ni eneo gani lina mapungufu na mchezaji gani anamhitaji,” amesema Kimbe.

Ameongeza kuwa kwa pesa walizonazo wana uwezo kabisa kusajili wachezaji wanaotoka Simba au Young Africans, lakini wale ambao wanawaniwa na timu hizo.

‘We subiri tu uone, utakuwa usajili wa kufuru, hatutaki tena mzaha, mchezaji kutoka Simba au Yanga sisi tunaweza kumsajili na hata anayewaniwa na timu hizo, tunaweza kutia mguu kumsajili, Mbeya City ya msimu ujao itakuwa moto,” amesema katibu huyo.

Akieleza sababu ya kutofanya vema msimu huu, mwenyekiti huyo alisema timu ilikuwa na wachezaji wengi chipukizi wasio na uzoefu wa ligi, lakini kubadili makocha mara kwa mara, na pia ikasajili wachezaji wengi wa dirisha dogo.

“Mimi niliingia madarakani bado mechi 10, timu ilikuwa na changamoto, lakini tunashukuru tumebaki, kikubwa hatutorudia tena hali hii,” amesema.

Mbeya City ilinusurika kwenye mechi ya mchujo dhidi ya Geita Gold, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini na kabla ya kushinda 1-0 nyumbani, hivyo kubaki Ligi Kuu.

Mlipuko Lebanon: Wafanyakazi 16 wakamatwa
Namungo FC wakwama usajili wa Ajibu, Mobby