Kiungo Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Bernard Morrison, ameendelea kuwasihi Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo kuwa na matumaini na kikosi chao ambacho kinashika nafasi ya pili kwenye Msimamo wa Ligi Kuu.

Morrison ametoa nasaha hizo, kufuatia Simba SC kutazamwa kama timu iliyopoteza muelekeo, hasa baada ya kuanza kwa kusuasua katika msimu huu wa 2021/22.

Kiungo huyo kutoka nchini Ghana amesema bado kikosi chao kina nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, hivyo amewataka Wanachama na Mashabiki kupuuza yanayosemwa kwenya mitandao ya kijamii.

Morrison amesema: “Ni kweli hatujawa na matokeo mazuri katika michezo yetu iliyopita msimu huu kulinganisha na wapinzani wetu, lakini niwahakikishie kuwa bado tuna muda wa kubadilisha hili na kama wachezaji tunafanya kila jitihada kuhakikisha tunapambana kutetea kombe letu msimu huu licha ya upinzani mkubwa ambao tunatarajia kukutana nao kutoka kwa wapinzani wetu.”

Tayari kikosi cha Simba SC kimeshashuka dimbani mara tano na kujikusanyia alama 11, huku Young Africans wakiwa kileleni kwa kuwa na alama 15, zilizotokana na kushinda michezo yao mitano.

Eddie Howe akabidhiwa mikoba Newcastle United
Ramos haondoki Paris Saint-Germain