Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso) limesema kuwa linataka uchunguzi wa haraka ufanyike, huku likitaja makundi matatu yanayopaswa kulaumiwa kwa kifo cha mwanafunzi Akwiline.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tahliso, George Mnali ambapo amedai kuwa makundi hayo hayawezi kukwepa lawama kuhusu kifo cha binti huyo kilichotokea Februari 16 kwa kuwa pasipo wao kuandamana asingefikwa na umauti.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amejibu tuhuma hizo kwa kusema kuwa anashangazwa na lawama zinazotolewa na shirikisho hilo akidai huenda wametumwa.

“Hawa ni wasomi gani ambao hawafahamu kuwa maandamano yapo kikatiba na Sheria ya Vyama vya Siasa inaruhusu jambo hilo. Nadhani wangejikita kujua chanzo cha maandamano na ningeona wako sahihi kama wangemuelekezea lawama hizo mkurugenzi wa Kinondoni aliyechelewesha kutoa hati za viapo kwa mawakala wetu,”amesema Mrema

Aidha, amehoji pia ni nini hasa kilichowachelewesha Tahliso kutoa tamko hilo hali ya kuwa tukio la mauaji ya Akwilina Akwilini limetokea wiki mbili zilizopita.

Hata hivyo, Akwilina aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza NIT, aliuwawa kwa kupigwa risasi eneo la Kinondoni Mkwajuni wakati polisi wakitawanya maandamano ya wafuasi wa Chadema wakiwa na viongozi wao waliokuwa wakielekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni kudai hati za viapo vya mawakala wake.

 

TRA kutoza kodi nyumba zisizo kamilika
Azam FC yafafanua kuhusu Al Masry kutumia basi lao