Mwanasiasa mkongwe nchini, na Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustino Mrema amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameweka historia ya mapambano ya uchumi nchini kutokana na namna ambavyo analishughulikia suala la madini.

Mrema ameeleza kushangazwa kwake na baadhi ya watu wakiwemo baadhi ya wabunge kutozipa uzito jitihada za Rais Magufuli za kutetea maslahi ya nchi.

“Baadhi ya wabunge wanaacha ajenda ya msingi ya kupambana na unyonyaji unaofanywa na makapuni ya madini badala yake wanaanzisha kampeni dhidi ya Rais” amesema Mrema.

Amesema Rais Magufuli yupo makini, amekuja na mpango anautekeleza, tumuunge mkono kwani sisi ndio tuliomchagua.

Mrema amesema kuwa kitendo cha Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Cooperation, Profesa John Thornton kusafiri kuja kuonana na Rais Magufuli na kukubali kuilipa Tanzania fedha zote ilizokoseshwa na Kampuni Acacia ni kielelezo kuwa sio tu kuwa ujumbe wake umefika lakini zaidi inadhihirisha kuwa madai yake dhidi ya kampuni hiyo ya uchimbaji madini ni ya msingi.

“Ni kiongozi gani barani Afrika aliyethubutu kuishutumu kampuni ya nje kama alivyofanya Rais Magufuli halafu viongozi wake wakasafiri kuonana na kiongozi huyo kutaka suluhu kama alivyofanya Mwenyekiti huyo wa Barrick kwa Tanzania?” amesema Mrema.

Amesema kuwa haiwezekani mtu mkubwa na mashuhuri atoke Canada kuja kuonana na Rais wetu tena akiwa na Balozi wa nchi yake iwe ni jambo la kupuuzwa.

Ameendelea kueleza kuwa tangu Rais Magufuli aunde tume za kuchukunguza Makinikia kumekuwepo na baadhi ya watu wanaopinga hatua hiyo kwa madai kuwa inaweza kuitia Tanzania katika mgogoro wa kisheria na kampuni ya Acacia.

Baada ya ripoti ya Kamati ya Pili ya Uchunguzi kuwasilisha taarifa yake kwa Rais Magufuli tumeona namna kampuni hiyo ilivyoikosesha Serikali trilioni za shilingi, hali iliyomfanya hadi mmiliki mkubwa wa kampuni hiyo, Profesa John kuja nchini kwa mashauriano na Rais.

Hivyo, Mrema amelikumbusha Jeshi la Polisi nchini wajibu wake wa kumlinda Rais dhidi ya kejeli za baadhi ya watu wakiwemo wabunge na kulitaka jeshi hilo kutofanya ajizi kuwakamata watu wanaofanya vitendo hivyo dhidi ya Rais na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

“Sheria ziko wazi kuhusu jambo hilo. Hata mimi mwenyewe niliwahi kushitakiwa mahakamani kwa kesi kama hiyo lakini nikashinda kwa kuwa waendesha mashitaka walishindwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa nilifanya kosa hilo” amesema Mrema.

Hamari Traore Apanda Daraja Ufaransa
Neno Kutoka Kwa Rais Wa TFF Kuelekea Uchaguzi Mkuu