Hatimaye Uongozi wa Mabingwa wa Soka nchini England ‘Manchester City’ umesaini mkataba Mpya na Meneja wa Klabu hiyo Pep Guardiola, baada ya kukamilisha mazungumzo yaliyodumu kwa siku kadhaa zilizopita.

Guardiola amesaini Mkataba Mpya Klabuni hapo, ambapo katika kipindi hiki atasalia Manchester City hadi mwaka 2025.

Guardiola mwenye umri wa miaka 51, ameshinda mataji 11, ambapo miongoni mwa Mataji hayo ya Ligi Kuu ya England yapo manne akitumika kwa miaka sita tangu alipotua Uwanja wa Etihad, akitokea kwa mabingwa wa Ujerumani FC Bayern Munich.

“Tangu siku ya kwanza nilihisi kitu maalum kuwa hapa. Siwezi kuwa mahali pazuri zaidi,”

“Nimefurahi sana kubaki Manchester City kwa miaka miwili zaidi.”

“Siwezi kusema neno la ahsante kwa kila mtu katika klabu hii kwa kuniamini hili ni letu sote. Nina furaha sana, na nina kila kitu ninachohitaji kufanya kazi yangu kwa ubora iwezekanavyo.”

“Najua kinachofuata katika klabu hii kitakuwa cha kushangaza kwa muongo ujao. Ilifanyika katika miaka 10 iliyopita, na itafanyika katika miaka 10 ijayo kwa sababu klabu hii iko imara.”

“Bado nina hisia kwamba kuna mengi zaidi tunaweza kufikia pamoja na ndiyo maana nataka kubaki na kuendelea kupigania mataji.”

Naye Mwenyekiti wa Manchester City Khaldoon Al Mubarak amesema “Nimefurahi kwa Guardiola kusaini mkataba mpya ambao utamuwezesha kuwa sehemu ya mafanikio ya Klabu hii.”

“Tayari amechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio na muundo wa Klabu hii, inafurahisha kufikiria nini kinaweza kutokea kutokana na nguvu, njaa na tamaa ambayo bado anayo,”

“Chini ya uongozi wake kama Mkuu wa Benchi la Ufundi Manchester City imetimiza mengi, huku ikiendelea kucheza na kubadilika mara kwa mara,”

Manchester City kwa sasa inashika nafasi ya Pili katika Msimamo wa Ligi Kuu ya England, ikitanguliwa na Arsenal iliyo kileleni kwa tofauti ya alama tano.

Mapema mwaka 2023, Klabu hiyo itaendelea na Mshike Mshike wa Ligi Kuu ya England, huku ikikabiliwa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya hatua ya 16 bora dhidi ya RB Leipzig ya Ujerumani.

Guardiola amewahi kupata mafanikio makubwa akiwa na klabu nyingine nguli Barani Ulaya kama FC Barcelona na FC Bayern Munich kabla ya kujiunga na City mwaka wa 2016.

Ndiye meneja aliyefanikiwa zaidi Barca akiwa na mataji 14 ndani ya miaka minne, yakiwemo mataji matatu ya La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa. Kisha akashinda mataji matatu ya Bundesliga mfululizo akiwa Bayern.

Mabehewa ya SGR katika muonekano halisi
Chomoka na Ndinga mpya msimu huu wa Kombe la Dunia