Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ameeleza sababu za kujiuzulu nafasi ya Uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii akiliweka jimbo lake mbele.

Nape ambaye uamuzi wake wa kujiuzulu nafasi hiyo ulizua mijadala mingi kwa kuzingatia kuwa ni Mwenyekiti wa tatu wa Kamati za Bunge kuchukua nafasi hiyo, amesema kuwa aliamua kujiuzulu ili apate nafasi zaidi ya kuwatumikia wananchi wake kwani muda uliosalia ni mchache ukilinganisha na majukumu aliyonayo jimboni kwake.

Kwa mujibu wa IPPp Media, Nape ameyasema hayo leo akiwataka  wananchi kuzingatia sababu alizozitoa yeye na kuachana na kile alichokieleza kuwa ni maneno ya barabarani.

Katika hatua nyingine, Nape ambaye amewahi kuwa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amekishauri chama chake kuzingatia kwa umakini kundi la vijana ambao ndilo lenye wapiga kura wengi kwani kundi hili haliijui historia ya chama.

“CCM ikiweza kuutafsiri ukuaji wa uchumi kutoka kwenye makaratasi kwenda kwenye maisha ya mwananchi, itawavutia vijana wengi watakaopiga kura mwaka 2020 kwakuwa itaboresha huduma za msingi ikiwemo maji, afya, barabara na nyinginezo,” IPP Media inamkariri Nape.

Taarifa za Nape kujiuzulu nafasi hiyo zilithibitishwa na Ofisi ya Bunge lakini sababu zilizoainishwa na Mbunge huyo hazikuwekwa wazi.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 7, 2019
Mawakili Njombe waomba kusogezewa Mahakama Kuu

Comments

comments