Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umekiri kuwa mradi wake wa ujenzi wa mji wa kisasa wa Dege Eco Village katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam wa shilingi trilioni 1.4 wanaoutekeleza kwa ushirikiano na kampuni ya Azimio Housing, ulijaa udanganyifu na ufisadi.

Akizungumza katika mkutano na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema kuwa kwa mujibu wa mkataba na masharti ya makubaliano ya ujenzi wa mji huo, NSSF inatakiwa kutoa asilimia 45 ya mtaji na Azimio inatakiwa kutoa jumla ya asilimia 55 ya mtaji ambapo asilimia 35 ni kwa fedha taslimu pamoja na ardhi ambayo ilithaminishwa kuwa asilimia 20 ya mtaji.

Kwa mujibu wa Profesa Kahyarara ambaye alishika nafasi hiyo tangu mwezi Machi mwaka huu, NSSF ilibaini kuwepo udanganyifu na uvunjifu wa masharti ya mkataba kwa kiasi kikubwa. Alitoa mfano kuwa eneo la ardhi ya mradi iliyotolewa na Azimio ni ekari 3,503 tu badala ya ekari 20,000 zilizopo kwenye mkataba.

”Gharama za mradi pia ziliongezwa tofauti na uhalisia, gharama ya ekari moja iliwekwa kuwa ni shilingi milioni 800 wakati kiuhalisia ekari moja ni shilingi milioni 25 tu,” alisema Profesa Kahyarara.

Baada ya kupitia na kusikiliza maelezo ya Bosi huyo wa NSSF, Kamati hiyo ya Bunge ilibainisha kuwa pande zote mbili zinahusika kwenye udanganyifu na ufisadi huo.

Akijibu swali la Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige aliyetaka kufahamu ni kwanini wasivunje mkataba na Azimio Housing kwa udanganyifu huo, Profesa Kahyarara alisema kuwa wakifanya hivyo wataingia hasara ya shilingi bilioni 270 kwa kuwa mkataba wao unawafunga.

Mwenyekiti wa PAC ambaye ni Mbunge wa Same Mashariki, Naghejwa Kaboyoka (Chadema) alitahadharisha kuwa suala hilo lazima lichukuliwe kwa uangalifu mkubwa kwa kuzingatia sheria ili kuepuka hasara kubwa zaidi inayoweza kujitokeza.

”Azimio bado ndio wamiliki wa ardhi na tayari NSSF wameshajenga majengo kadhaa pale. Kama NSSF itajitoa kwa haraka, inaweza kuelezwa na mahakama kuondoa majengo yake kwenye ardhi hiyo,” Kaboyoka anakaririwa.

Makala: Ali Kiba ajifunze haya kwa Diamond na Diamond afuate haya kwa Kiba
Real Madrid Wafanya Kweli, Wamuwekea Uzio Vázquez