Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin ametoboa siri ya mabadiliko ya Kiungo Mshambuliaji Bernard Morrison.

Morrison aliisaidia Simba SC kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Red Arrows ya Zambia, katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa Jumapili (Novemba 28), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kocha Pablo amesema alichokifanya ni kutoa nafasi kwa kiungo huyo kucheza kwa uhuru tangu kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting, uliomalizika kwa Simba SC kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kocha Pablo amesema: “Morrison akicheza akiwa huru uwanjani atakuwa akitengeneza nafasi nyingi za kufunga kama ile ya Meddie Kagere, atafunga mwenyewe, mabeki watamchezea rafu na kupata penati au faulo ambazo tutazitumia kupata mabao.”

“Naamini Morrison ni moja ya wachezaji hatari zaidi wakati tukiwa na mpira muda ambao tunashambulia ila kuna vitu vingine vya kiufundi nitamuongezea zaidi.”

“Ukiangalia katika kikosi changu kwa sasa sio Morrison tu ambaye ndio amekuwa bora bali hata wachezaji wengine wamezidi kuimarika kulingana na majukumu ya nafasi zao.”

Simba SC kesho Jumatano (Desemba Mosi) itarejea tena Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kucheza dhidi ya Geita Gold, kucheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Minziro: Tumejiandaa kuikabili Simba SC
Rihanna awa Shujaa wa Barbados