Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai amefanya mabadiliko  madogo ya wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge, huku akiwapangia kamati waliokuwa mawaziri ambao wametenguliwa.

Aidha Taarifa hiyo imetolewa leo Oktoba 9, 2021 na ofisi ya Spika yakihusisha wabunge saba wakiwemo waliokuwa mawaziri watatu ambapo mabadiliko hayo yamefanyika kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni ya 135 (3) – (5) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Juni 2020.

Mbunge wa kuteuliwa, Humphrey Polepole amehamishiwa kutoka kamati ya utawala na Serikali za mitaa kwenda kamati ya sheria ndogo, kuhamishwa kwa polepole kunamfanya kupoteza nafasi yake ya uongozi wa kamati uliokuwa unamfanya kuwa mjumbe wa kamati ya uongozi inayohusisha wenyeviti wote wa kamati za kudumu za Bunge ambapo mwenyekiti wake ni Spika.

Mabadiliko mengine ambayo Spika ameyafanya ni kumhamisha Godwin Kunambi kutoka kamati ya mambo ya nje, ulinzi na usalama kwenda kamati ya ardhi, maliasili na utalii.

Spika pia amewateua baadhi ya wabunge katika kamati kadhaa ambapo Asia Halamga na Agnes Marwa wamepelekwa kamati ya masuala ya Ukimwi.

Pia, amemteua Dkt. Faustine Ndugulile kuwa mjumbe wa kamati ya sheria ndogo na kamati ya masuala ya Ukimwi Dkt. Medard Kalemani na Dk Leonard Chamuriho wameteuliwa kuwa wajumbe wa kamati ya sheria ndogo.

Polepole amjibu Spika Ndugai
Mfahamu Abdulrazak Gurnah: Mwanafasihi aliebeba kidedea Tanzania Ulimwenguni