Serikali imepanga kuwasaka na kuwawajibisha watu wote waliokuwa wakipokea fedha zilizotokana na watumishi hewa baada ya kukamilisha zoezi la utambuzi.

Hayo yamesemwa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jijini London nchini Uingereza alipokuwa akizungumza na Watanzania waishio nchini humo kwenye mkutano uliofanyika katika Ubalozi wa Tanzania jijini humo.

“Wafanyakazi hewa wamefikia zaidi ya 10,000 na tumeokoa zaidi ya shilingi bilioni 4.5 zilizokuwa zikipotea kila mwezi. Tukikamilisha zoezi la kusaka watumishi hewa, sasa tutataka kujua ni akina nani walikuwa wakipokea fedha hizo. Waliohusika tutashughulika nao,”  alisema Waziri Mkuu.

Aliongeza kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha inakuwa na watumishi ambao wanafanya kazi kwa kuzingatia misingi ya uaminifu, uadilifu na uwajibika mahali pa kazi.

Waziri Mkuu alieleza kuwa Serikali imejikita katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ili kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anafaidika na raslimimali zilipo nchini kwa haki.

“Jambo tuliloamua kuanza nalo ni kupambana na rushwa. Tumeamua kufanya hivyo ili kurudisha umoja na maelewano miongoni mwa Watanzania, tunataka tuibadili Tanzania ili iwe ni ya Watanzania wote… tumechoka kuambiwa sehemu fulani mradi umekamilika halafu ukienda kuangalia hukuti kitu na fedha ile haipo,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka watanzania hao kuwaalika marafiki zao ambao ni watu makini ili waweze kuwekeza nchini kwani kuna fursa kubwa ya uwekezaji hususan katika sekta ya kilimo.

Alisema kuwa Serikali inataka usindikaji wa mazao na bidhaa ufanyike nchini ili kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania na kuepuka kusafirisha mazao ghafi.

Waziri Mkuu alikuwa jijini London alipoenda kumuwakilisha Rais John Magufuli katika mkutano wa Kimataifa uliojadili mapambano dhidi ya Rushwa.

 

 

Jaji Mkuu aipigia mstari Sheria ya Makosa ya Mtandao na uhuru wa kupata taarifa
Mkuu wa Wilaya awakwepa vigogo waficha sukari, aogopa kuwekwa mitandaoni