Serikali, imetoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa UVIKO-19, na kusema katika kipindi cha Julai 2 hadi 29, 2022 jumla ya visa vipya vya maambukizi 543 vimethibitika ikilinganishwa na visa 352 kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita kwa kuanzia Juni 4 hadi Julai 1, 2022, sawa na ongezeko la asilimia 54.3.

Kwa mujibu wa taarifa, iliyotolewa kwa umma na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifello Sichalwe imesema katika kipindi hicho, hakuna kifo kilichotokea kutoka na UVIKO 19 na kwamba mchanganuo wa takwimu katika kipindi cha tarehe Julai 2 – 29, 2022 unaonesha watu waliothibitika kuwa na ugonjwa huo walitoka Mikoa ya Dar es Salaam (366) na Mwanza (41).

Mikoa mingine ni pamoja na Mbeya (24), Shinyanga (20), Katavi (19), Arusha (16), Lindi (13), Kilimanjaro (12), Mtwara (12), Mara (7), Simiyu (5), Tabora (2), Kagera (2),
Morogoro (2), Iringa (1) na Dodoma (1).

Aidha, taarifa ya Dkt. Sichalwe imesema, “Jumla ya wagonjwa kumi (10) waliothibitika kuwa na UVIKO-19 walilazwa na wote walikuwa hawajapata chanjo. Hali hii inaashiria
kuwa maambukizi yameongezeka katika jamii ikilinganishwa na mwezi mmoja uliopita.”

Amesema, Serikali imeendelea kutoa chanjo ya UVIKO-19 nchini, ili kuwawezesha wananchi kupata kinga na kwamba kuanzia Julai 2 – 29, 2022 jumla ya Wananchi waliopata dozi kamili ya chanjo hiyo ni 4,223,670, ikiwa ni ongezeko la watu 1,182,519 ikilinganishwa na kiwango cha uchanjaji katika mwezi mmoja uliopita ambapo watu 3,041,151 walichanja.

“Wizara inaendelea kuwahimiza wananchi kupata na kukamilisha dozi za chanjo ya UVIKO-19 ili kuzuia kupata ugonjwa mkali hata kusababisha kifo, pale mtu anapopata maambukizi,” imesema taarifa hiyo ya Dkt. Sichalwe.

Hata hivyo, amesema Wizara inatoa tahadhari kwa wananchi wote kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na UVIKO – 19 ikiwa ni pamoja na kupata kwa wakati dozi kamili za chanjo ya UVIKO – 19 na kuvaa barakoa pindi unapojisikia dalili za mafua na kwenye mikusanyiko ya ndani ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi.

Tahadhari nyingine ni pamoja na kuzingatia usafi binafsi ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutumia vipukusi (sanitizer) mara kwa mara, kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya endapo utakuwa na dalili za ugonjwa huo na kuendelea kuchukua hatua za kujenga mwili imara kwa kufanya mazoezi na kula vyakula bora.

Aidha, amesema Wananchi pia wanapaswa kutoa taarifa za kuwepo watu wenye dalili za ugonjwa huu katika jamii kupitia namba ya simu ya bure ya 199.

Kenya: Wanaharakati wawafikisha Ruto na Gachagua Mahakamani
Kenya: IEBC yapunguza kura elfu 10 za Ruto