Licha ya kuhusushwa na taarifa za kutarajiwa kuishusha moja ya klabu kubwa Barani Afrika kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaonogesha Tamasha la Simba Day, Uongozi wa klabu hiyo umeendelea kuwa kimya na kuwataka Mashabiki na Wanachama kuwa watulivu

Simba SC ambao wanatarajia kufanya Tamasha lao (Simba Day) Septemba 19, Uwanja wa Benjamin Mkapa wanatajwa kuialika Klabu Bingwa Barani Afrika kwa sasa Al Ahly kutoka nchini Misri.

Mwenyekiti wa klabu hiyo Murtaza Mangungu amesema bado wanaendelea na maandalizi ya Tamasha hilo, na ni mapema mno kutangaza kikosi chao kitapambana na timu gani siku hiyo.

Mangungu amesema Wanachama na Mashabiki wa Simba SC wanatakiwa kusubiri na kuuamini Uongozi wao kuwa utawaletea timu kubwa, itakayowapa burudani siku ya Tamasha la Simba Day.

“Kwa sasa hatuwezi kuweka wazi kuhusiana na uratibu wa tukio letu la Tamasha la Simba kwa kuwa bado tunaendelea na maandalizi, tutaweka wazi kila kitu pale muda utakapokuwa tayari.

“Lakini naloweza kukuthibitishia ni kuwa tutaalika timu moja kubwa kutoka nje ya nchi, tupo kwenye mazungumzo na timu kubwa hapa Afrika kama Al Ahly, Zamalek, Horoya ili kuangalia uwezekano wa wao kupata nafasi ya kuja kwenye tamasha hilo.”

Uongozi wa Simba SC hulitumia Tamasha la Simba Day, kutambulisha wachezaji wapya waliosajiliwa kwa msimu unaofuata, burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali na kucheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki.

Uzinduzi wa Jezi mpya Simba SC Septemba 04
Joe Biden: Kuondoa majeshi ya Marekani ni uamuzi bora