Bunge la Somalia jana Jumamosi lilipiga kura ya kumtoa madarakani Waziri Mkuu Hassan Ali Khaire, ambaye amekuwa akikosolewa kuhusu udhaifu wake katika kutatua matatizo ya usalama nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa, wabunge wamepiga kura ya kutokuwa na imani na Hassan Ali Khaire kwa kura 170 na wabunge wanane wamepiga kura ya hapana.

Spika wa Bunge la Somalia Mohamed Mursal Sheikh Abdirahman amesema waziri mkuu ameshindwa kuanzisha kikosi cha kitaifa kwa ajili ya usalama wa serikali ya kitaifa na serikali za majimbo. Magaidi wa Al Shabab wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara Somalia na hivyo kuvuruga mchakato wa kurejesha usalama wa kudumu nchini humo.

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed amesema katika taarifa kwamba anakubali uamuzi wa bunge wa kumtimua waziri mkuu na kwamba hivi karibuni atamteua waziri mkuu mpya.

Khaire ambaye ni raia pacha wa Somalia na Norway aliwahi kuwa mwalimu wa shule ya msingi nchini Norway na pia mfanyakazi wa Baraza la Wakimbizi la Norway kabla ya kufanya kazi katika sekta ya mafuta ya petroli.

Khaire aliteuliwa kuwa waziri mkuu mwaka 2017, mapema mwezi huu alisema uchaguzi wa bunge Somalia unapaswa kufanyika mwaka huu kabla ya muhula wa sasa wa bunge kumalizika Disemba. 

Tume ya uchaguzi ya Somalia bado haijatangaza ratiba ya uchaguzi na imekuwa ikipendekeza uchaguzi ufanyike mwaka ujao kutokana na kuchelewa zoezi la kujitayarisha. Uchaguzi wa rais wa Somalia nao pia umepengwa kufanyika Februari mwakani.

Picha: Viongozi wakiaga mwili wa Mkapa uwanja wa uhuru
Familia yasema ugonjwa uliomwondoa Mkapa