Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inashuka dimbani hii leo dhidi ya Kenya katika mchezo wa pili wa makundi wa michuano ya AFCON.

Mchezo huo unaotarajia kupigwa majira ya saa 5:00 usiku wa leo, unatarajia kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ukaribu wa mataifa haya mawili na historia ya michezo yao ya nyuma.

Timu hizi zimekutana zaidi ya mara 50 mpaka sasa katika mashindano mbalimbali, ambapo mchezo wa kwanza kuzikutanisha timu hizo ni Septemba 25, 1971, ambapo mchezo huo ulimalizika kwa kufungana bao 1-1. Kisha miaka 20 ikapita baada ya hapo kabla ya kukutana katika mchezo wa pili mnamo 11 Novemba 1991 na kumalizika kwa sare ya 1-1.

Katika michezo yote ambayo imezikutanisha timu hizo, Kenya ‘Harambee Stars’ imefanikiwa kushinda kwa zaidi ya asilimia 48, huku Taifa Stars ikishinda kwa asilimia 32 na asilimia 20 timu hizo zikitoka sare.

Aidha, Mchezo wa mwisho wa kimashindano kuzikutanisha timu hizo ni 11 Disemba mwaka 2017 katika michuano ya CECAFA, mchezo ambao Kenya iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Kwenye michuano ya AFCON inayoendelea nchini Misri, timu zote zimepoteza mchezo wa kwanza, Taifa Stars ikifungwa mabao 2-0 na Senegal, huku Harambee Stars ikifungwa 2-0 na Algeria. Hali hiyo inaufanya mchezo huu kuwa ni wa muhimu zaidi kwa timu zote mbili ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele.

Bodi ya BASATA yaitisha mkutano mkubwa na Wasanii wote Nchini
Bashe ang'aka, 'Hili genge la wahuni ipo siku nitawataja kwa majina'

Comments

comments