Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Mkuchika amesema kuwa Tanzania inaendelea kupata heshima kubwa katika Jumuiya ya Kimataifa katika vita vya mapambano dhidi ya rushwa kutokana na mshikamano na nguvu ya pamoja iliyopo katika vyombo na taasisi zinazosimamia utawala bora nchini.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam katika kongamano la siku maalum dhidi ya rushwa katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba, ambapo amesema kuwa utafiti uliofanywa na taasisi hizo zimesifu juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano na kuitaja Tanzania kuwa ni nchi ya mfano katika vita vya mapambano dhidi ya rushwa.

Amesema kuwa taasisi hizo zikiwemo MO Ibrahim, Transparency International, APRM na taasisi nyingine kubwa duniani zinazosimamia masuala ya utawala bora zimefanya utafiti na kusifu juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika mapambano dhidi ya rushwa ambapo tafiti mbalimbali zimeifanya Tanzania kushika nafasi ya pili nyuma ya nchi ya Rwanda.

”Kwa sasa vyombo vyetu vyote serikalini si TAKUKURU pekee bali pia polisi, tiss (usalama wa taifa), Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ICAG) na vingine vyote, vimeendelea kuunga katika kusimamia masuala ya utawala bora na hili limeleta msukumo na hamasa mpya katika vita dhidi ya rushwa hapa nchini,”amesema Mkuchika

Akizungumzia rushwa katika sekta ya viwanda na biashara, Waziri Mkuchika amesema kuwa Serikali imeendelea kuweka mikakati mbalimbali katika kupunguza tatizo hilo ambalo limekuwa likiathiri sekta binafsi ambayo imekuwa mshirika wa karibu wa serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, rushwa katika sekta ya biashara imekuwa ikiathiri sana masuala ya uwekezaji wa kigeni, ambapo eneo lililoonyesha kutawala kwa rushwa ni katika eneo la utoaji wa vibali na leseni kutoka katika taasisi na Idara muhimu za serikalini na hivyo serikali imeendelea kulifanyia kazi ili kuhakikisha kuwa vikwazo hivyo vinaondolewa kwa wawekezaji na hivyo kuharakisha ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Diwani Athumani amesema kuwa serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kupitia Mpango Mkakati dhidi ya mapambano ya rushwa (NASCAPIII) ili kuhakikisha kuwa mapambano na vita dhidi ya rushwa yanapata mafanikio nchini.

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 4, 2019
Mkuu wa wilaya ya Makete asema yupo salama, amaliza kugawa Vitambulisho