Baada ya kuambulia alama moja kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, mshambuliaji kutoka Tanzania, Thomas Ulimwengu na wenzake watakuwa na kibarua kizito huko Sudan kupigania pointi tatu za kwanza katika hatua ya makundi dhidi ya Al-Hilal Omdurman.

Ulimwengu na mastaa wenzake wa TP Mazembe walichemka katika mchezo wa kwanza ambao ulipigwa Lubumbashi na kuambulia alama hiyo moja huku wenzao, Al-Hilal Omdurman. wao wakikiona chamoto Afrika Kusini, walichezea kichapo cha mabao 2-0.

Katika mchezo huo, ambao utachezwa kesho Jumatano, Februari 24 atashuhudiwa Ulimwengu akirejea nyumbani, Omdurman kutokana na miaka ya nyuma kuichezea miamba hiyo ya soka la Sudan kabla ya kupata dili la kujiunga na JS Soura ya Algeria.

Bila shaka kocha wa TP Mazembe, Pamphile Mihayo Kazembe anaweza kumtumia Ulimwengu mwenye mabao matatu kwenye mashindano hayo kama silaha yake muhimu kwenye kikosi cha kwanza kutokana na mshambuliaji huyo kuifahamu vizuri Al-Hilal Omdurman.

Al-Hilal Omdurman iliifunga TP Mazembe bao moja kwa sifuri kwenye michuano ya Simba Super Cup iliyounguruma jijini Dar es salaam mwezi Januari, na wenyeji Simba SC kuibuka mabingwa wa michuano hiyo.

Afya ya Waziri Mpango yaimarika
Chuo Kikuu cha SAUT kuzindua SAUT Alumni