Rais wa Marekani, Donald Trump amekataa ombi la msichana Mmarekani mwenye umri wa miaka 24, aliyekuwa amejiunga na kundi la kigaidi la Islamic State (IS) nchini Syria, la kutaka kurejea nyumbani.

Hoda Muthana, aliondoka Marekani akiwa na umri wa miaka 20, akaelekea Syria ambapo alijiunga na kundi hilo hadi mwaka huu lilipotawanywa rasmi na majeshi ya Marekani kwa kushirikiana na nchi washirika.

Familia ya Muthana imeeleza kuwa alipokuwa anaondoka kwenda Syria aliwadanganya kuwa alikuwa anaenda nchini Uturuki kuhudhuria tukio la chuo kikuu alichokuwa anasoma.

Trump ameandika kupitia akaunti yake ya Twitter kuwa amemuelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuwa msichana huyo sio tena raia wa Marekani.

Mwanasheria wa familia ya Muthana ameeleza kutokubaliana na tamko la Trump akidai kuwa ni jaribio la kuwanyang’anya Wamarekani uraia wao halali.

“Utawala wa Trump unaendelea kujaribu kuwavua uraia kimakosa wananchi wake. Honda Muthana ana hati halali ya kusafiria ya Marekani. Alizaliwa Hackensack, NJ, Oktoba 1994, miezi michache tu tangu baba yake alipoacha kuwa mwanadiplomasia,” mwanasheria Hassan Shibly aliiambia ABC.

Alisisitiza kuwa sio sahihi kuwavua uraia wananchi kwa sababu tu wamevunja sheria.

Suala la Muthana linafanana na kilichomkuta Shamima Begum, msichana ambaye ni raia wa Uingereza aliyejiunga na kundi la IS akiwa na umri wa miaka 15 tu, lakini sasa anataka kurejea tena nyumbani. Serikali ya Uingereza imekataa ombi la msichana huyo ambaye ana mtoto mdogo aliyempata akiwa nchini Syria.

Trump amewahi kuzisihi nchi za Ulaya kutowapokea watu ambao wamejisalimisha kutoka kwenye kundi la IS na kwamba watakapotaka kurejea nyumbani wakamatwe, wafungwe jela.

Mbunge wa Geita Mjini alilia umeme wa REA
Museveni kuitawala Uganda milele

Comments

comments