Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amewataka watendaji wa Sekta ya Uchukuzi kufanya kazi kwa uzalendo na weledi katika usimamizi wa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano ili kuleta maendeleo nchini.

Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa Sekta hiyo na kusema kuwa Serikali inawekeza fedha nyingi katika miradi mikubwa ikiwemo ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), ukarabati na ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge) hivyo, haitamvumilia Mtendaji yoyote atakayehujumu miradi hiyo.

“Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuwekeza fedha nyingi kwenye Sekta hii, hivyo ifike mahala tufikirie kusimamia miradi hii kwa uadilifu na uzalendo kwani uongozi unahitaji malengo ili kufanikisha utekelezaji’, amesema Mhandisi Kamwelwe.

Aidha, amesema kuwa Serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimeibuliwa na wadau wa usafirishaji katika utekelezaji wa Sheria mpya ya Uzito wa magari na kusema kuwa Serikali haitarudi nyuma juu ya sheria hiyo kwani inafanya hivyo ili kuilinda miundombinu ya barabara nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, amesema kuwa Watendaji wako tayari kuhakikisha wanasimamia miradi inayotekelezwa chini ya sekta ya uchukuzi ili iweze kudumu na kukuza uchumi wa nchi.

Mhandisi Chamuriho, ameeleza katika mwaka wa fedha wa 2019/20 Sekta imefanikiwa kukamilisha miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Gati namba 1 mpaka 7 katika bandari ya Dar es Salaam, Ujenzi wa gati namba 2 Bandari ya Tanga, Ujenzi wa jengo la tatu la Abiria katika Kiwanjja cha Ndege cha Mwl Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA), Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa Kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na Morogoro mpaka Makutupora jijini Dodoma, ujenzi wa rada 4 katika kiwanja cha ndege cha JNIA, Mwanza, Kilimanjaro na Mbeya.

Hata hivyo, baraza hilo la siku moja limewakutanisha watendaji mbalimbali wa Sekta ya Uchukuzi ambapo katika kikao hicho walijadili na kupitia utekelezaji wa bajeti ya 2019/20 na kupitisha bajeti ya zaidi ya shilingi trilioni 3 ambazo zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya sekta ikiwemo ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Viktoria, Ujenzi wa reli ya Kisasa Dar es Salaam-Morogoro, Morogoro-Makutupora unaondelea, uboreshaji wa shirika la ndege la Tanzania na ujenzi wa rada za kupima hali ya hewa.

Sababu vifo vya ghafla yatajwa
ACT- Wazalendo yawachimba biti viongozi wake Njombe

Comments

comments