Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amevitaka vyama vya Chadema na CCM kusitisha kampeni za ubunge katika majimbo ya Siha na Kinondoni kufuatia kifo cha mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru.

Zitto alikumbuka mchango wa Kingunge katika kuimarisha vyama vya CCM na Chadema kwa nyakati tofauti na kwamba hiyo ni sababu tosha kwa vyama vyote kuchukua uamuzi huo.

“Kingunge alisaidia kuimarisha CCM na baadaye akaiimarisha Chadema. Sioni busara kwa vyama hivi kuendelea na kampeni. Nawaomba wasitishe kampeni leo na kesho, Jumatatu mwanasiasa huyu akizikwa wataendelea,” Mwananchi inamkariri Zitto.

CCM na Chadema wanaendelea na kampeni za uchaguzi mdogo katika majimbo hayo ambako uchaguzi unatarajiwa kufanyika Februari 17 mwaka huu.

Mzee Kingunge ambaye alikuwa mmoja wa waasisi wa CCM akiwa na kadi namba nane, alitangaza kukihama chama hicho Oktoba mwaka 2015 akipinga utaratibu uliotumika kumuondoa Edward Lowassa kwenye orodha ya majina matano yaliyopigiwa kura kumpata mgombea urais.

Baada ya hatua hiyo, Kingunge alitangaza kuunga mkono umoja wa vyama vitano vya upinzani ulioitwa Ukawa, ukimsimamisha Lowassa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema.

Alifariki dunia Februari 2 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa anapatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kung’atwa na mbwa wake.

Mzee Kingunge atazikwa Februari 5 mwaka huu katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Yalivyoandikwa magazeti ya nje na ndani ya Tanzania leo
Video: Idadi ya wanaume wanaofanyiwa ukatili na wake zao yaongezeka