Bila shaka utakuwa unaikumbuka Filamu ya “The God Must Be Crazy”. Filamu hii muhusika mkuu alikuwa ni Nǃxau ǂToma, yeye alizaliwa eneo linalofahamika kama Tsumkwe, Namibia, (zamani ilikuwa ni sehemu ya South Africa).

Mpaka anafariki mwanzoni mwa miaka ya 2000 N!xau alikuwa hana kumbukumbu halisi ya umri wake na mwaka aliozaliwa lakini wajuaji walimkadiria kwamba eti alizaliwa 1944.

Baada ya kushiriki kama mhusika mkuu katika filamu ya “The Gods Must Be Crazy” 1980 chini ya muongozaji Jamie Uy’s, N!xau alianza kupata umaarufu mkubwa si tu Afrika, bali Duniani kwa ujumla.

Lakini licha ya filamu hiyo kuingiza kiasi cha zaidi ya dola za Kimarekani Milioni 60, inadaiwa Bwana huyo alilipwa dola 300 pekee na hivyo waandaaji kuingia katika shutuma toka kwa wafuasi wa N!xau.

Hata hivyo, mtengenezaji wa Filamu hiyo Jamie Uy’s alijitetea hadharani kwamba N!xau alizaliwa kuigiza na kwa hilo walifauli lakini kutokana na tamaduni zao hawakuona wala kujua thamani ya pesa.

Anasema, baada ya  kulipwa fedha hizo, (dola 300), aliziangalia kwa mshangao kisha aliziachia zikapeperushwa na upepo na yeye kuondoka kuendeleza mipango yake ya kila siku.

Maneno ya Muongoza filamu huyo yanadaiwa kwamba yalikuwa na uhalisia kwani jamii ya N!xau haikutumia pesa, wao waliwinda, walifuga na waliishi kwa msaada wa Serikali ya Afrika ya Kusini.

Inaarifiwa kuwa baada ya kushiriki filamu ya The Gods Must Be Crazy, N!xau alitembea maeneo mengi duniani. hapo aliona na kutambua namna dunia iliyostaarabika na katika kazi mbali mbali za filamu alizoigiza baadaye alilipwa hadi dola za Kimarekani 500,000.

The Gods Must Be Crazy ya mwaka 1980, ilimtoa na baadaye alionekana katika filamu nuingine ya The Gods Must Be Crazy sehemu ya pili mwaka 1989, halafu akaonekana tena katika Crazy Safari 1991 na Crazy Hong Kong 1993, kisha The Gods Must Be Funny in China ya 1994.

Hata hivyo, baada ya kumaliza uigizaji kwa miaka kumi nje N!xau aliomba kurejea  nyumbani na Fedha alizozipata alizitumia kujenga nyumba ya matofali, aliweka umeme nyumbani kwake, pampu ya maji kufuga baadhi ya mifugo baada ya kurejea katika ardhi yake.

Inaarifiwa pia aliwahi kununua gari  lakini hata hivyo hakuweza kulimudu kwani hakujua kuendesha na hakua na uwezo wa kumlipa dereva hivyo akaachana nalo na kuendeleza yale aliyoyamudu.

Katika hali isiyo ya kawaida, N!xau alikutwa amefariki kando na mji wake mara baada ya kuaga kwamba anakwenda kusenya kuni na ingawa chanzo cha kifo chake hakikujulikana watu wake wa karibu wanadai alikua akisumbuliwa na Kifua kikuu.

Julai 12, 2003,Nǃxau ǂToma alipumzishwa katika nyumba yake ya milele huko Tsumkwe akiacha Watoto sita na historia kubwa ambayo ni vigumu kusahaulika katika ulimwengu wa filamu Duniani.

 

Bila amani hakuna maendeleo - Rais Dkt. Mwinyi
Makala: Gari la Maziwa chanzo mistari ya Barabarani