Usajili wa Mlinda Lango mpya wa Mtibwa Sugar, Justin Ndikumana, umeelezwa utamwongezea nguvu Mohamed Makaka ambaye anatumika sana na kukumbwa na majeraha ya mara kwa mara.
Kocha wa makipa wa timu hiyo, Patrick Mwangata amesema ujio wa Ndikumana ni msaada mkubwa ndani ya kikosi hicho, hasa wakati huu timu hiyo inaburuza mkiani, ikicheza mechi 14 imeshinda mbili, sare mbili, imefungwa 10 na imefungwa mabao 29, imefunga 14 na kumiliki pointi nane.
“Ndikumana tangu atue nchini kuichezea Coastal Union alionyesha kiwango kikubwa sana, isitoshe anaaminiwa na timu yake ya taifa ya Burundi na yupo nayo muda huu,”
“Akitoka kwenye majukumu yake ambako watacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Algeria itakayopigwa leo Jumanne (Januari 09) Togo, atajiunga na sisi moja kwa moja kambini,” amesema Mwangata
Amesema katika timu yao walikuwa na makipa watatu, Makaka ambaye ni mzoefu na wawili waliowapandisha kikosi B ambao ni Toba Kutisha na Razack Shekimweri.
Kwa upande wa Ndikumana amesema kama kocha wa Mtibwa, amezungumzia usajili wake, hana budi kukiri ni kweli atajiunga nao, akitoka kwenye majukumu ya taifa.
“Sina nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo, kutokana na majukumu yaliopo mbele yangu, nadhani nikirejea Tanzania nitapata wakati mzuri wa kuzungumzia hilo kwa mapana,” amesema.