Mamlaka za Kongo Kinshasa na Kongo-Brazzaville zimesema watu 300 wamepoteza maisha, huku kaya 300,000 zikiharibiwa tangu wiki iliyopita kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na kupanda kwa kiwango cha maji ya Mto Kongo.
Mtaalamu wa masuala ya mito na maji nchini DRC, Ferry Mowa amesema ofisi yake ilitoa tahadhari ya kupanda kwa kiwango cha maji Desemba 2023 na ikatoa tahadhari kwa kuwa ukanda mzima wa mto Congo ungeweza kuathirika na mafuriko lakini hawakut8liwa maanani.
Inaarifiwa kuwa, katika nchi jirani ya Kongo Brazaville, jiji la Brazzaville ambalo linapitiwa na mto Congo mafuriko yalifababisha watu 17 kupoteza maisha na nyumba zaidi ya 60,000 kuathiriwa.
Wizara inayoshughulikia masuala ya kijamii nchini DRC, imesema vitongoji kadhaa katika mji Mkuu wa Kinshasa wenye idadi kubwa ya watu, vimeathirika pamoja na jamii nyingine zilizopo pembezoni mwa mto huo.
Waziri wa masuala ya kijamii na misaada ya kibinadamu nchini humo, Modeste Mutinga, alisema watatoa matokeo ya tathmini ya uharibifu na aina ya misaada ya kibinadamu inayohitajika mara baada ya kikao cha Januari 11, 2024.
Hata hivyo, ubovu wa miundombinu na upangaji holela wa miji unatajwa kuwa sababu kuu inayopelekea baadhi ya Mataifa ya kiafrika kukumbwa na mafuriko makubwa ya mara kwa mara, kutokana na mabadiliko ya tabianchi.