Mlinda Lango wa timu ya taifa ya Nigeria, Stanley Nwabali amewapongeza wachezaji wenzake kwa kuonyesha kiwango bora na kuisaidia timu kutinga hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika ‘AFCON 2023’.

Nwabali alipangua mikwaju miwili ya Penati wakati timu yake ikipambana na Afrika Kusini, mchezo uliochezwa Uwanja wa Bouake, lvory Coast na timu yake kuibuka na ushindi wa Penati 4-2 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika dakika 120.

Kipa huyo alisema kuwa siri ya kupangua mikwaju miwili ya Penati ni utulivu aliokuwa nao langoni katika mchezo huo.

Alisema anawapongeza wachezaji wenzake kutokana na kujituma kwa kiasi kikubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho na kuhakikisha timu yao inatinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

“Ninawapongeza wachezaji wenzangu kwa kuonyesha kiwango bora katika mchezo wetu dhidi ya Afrika Kusini, kwani kila mmoja alijituma kadri ya uwezo wake na kuhakikisha timu inatinga fainali za AFCON msimu huu, kitu ambacho tumefanikiwa,” alisema Nwabali.

Kipa huyo anayeidakia Chippa United ya Afrika Kusini, alisema pia anaupongeza uongozi mzima chini ya Kocha Jose Peseiro ambapo walikuwa wakionyesha ushirikiano kabla ya michuano hadi walipofika fainali.

“Wakati kocha amekuja kunitembelea hapo awali nilijisikia faraja kutokana na maneno ya kunipa moyo aliyonipatia kipindi tupo nyumbani.

“Kwangu kilikuwa kitendo kikubwa na cha heshima kutembelewa na kocha na kila alichoniambia nimekitekeleza na kuhakikisha ninaifikisha timu ilipo sasa,” alisema.

Alisisitiza kwamba ana imani mashabiki wa timu hiyo wamefurahia kwa kiasi kikubwa kuiona timu yao ikitinga fainali za AFCON  mara nyingine.

Alisema mchezo huo umeweka historia kwao na utakumbukwa na vizazi vijavyo kutokana na kiwango walichokionyesha.

Nigeria inatarajia kupambana na wenyeji lvory Coast katika fainali itakayopigwa keshokutwa Jumapili (Februari 11) katika Uwanja wa Olympic Ebimpe nchini humo.

Picha: Rais Samia ampokea Rais wa Poland Ikulu
Thamani ya Vitor Roque kupanda maradufu