Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kwa mwaka 2024 Shirika la Fedha Duniani (IMF) limesema kuwa Tanzania inatarajia kuwa kati ya nchi 20 zenye uchumi unaokuwa kwa kasi duniani.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imeeleza kuwa Rais Samia amesema hiyo ni fursa kwa wawekezaji wa Norway nchini Tanzania, kwani ina mazingira mazuri ya kisiasa, kijiografia na kiuchumi.

Aliyabainisha hayo wakati akihutubia Mkutano wa Jukwaa la Biashara kati ya nchi hizo mbili, uliofanyika jijini Oslo, Rais Samia amebainisha zipo kampuni kadhaa za Norway zilizotumia fursa hiyo vizuri kwa uchumi wa Tanzania.

Aidha, Rais Samia amesema kisiasa Tanzania ina amani chini ya demokrasia imara kwa mfumo wa vyama vingi wenye kuzingatia tunu za utawala bora, kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

Kwa upande wa kijiografia, Rais Samia amesema Tanzania inafaa kwa uwekezaji kwani ina Bandari ya Dar es Salaam katika Bahari ya Hindi, inayohudumia mataifa manane ya Afrika inayopakana nayo.

 

Kiuchumi, amesema Tanzania ina sera nzuri na imara za kiuchumi na kifedha huku ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) ukirejea kwenye asilimia  5.2 kwa mwaka. Unatarajiwa kufikia zaidi ya asilimiq 6 kwa mwaka ujao kama ilivyokuwa kabla ya COVID 19.

Aidha, amesisitiza fursa tano za kipaumbele zikiwemo uwekezaji katika nishati mbadala, kilimo, mafuta na gesi, mifuko ya uwekezaji, miundombinu na usafirishaji.

Rais Samia ameanza ziara ya Kitaifa nchini Norway kwa muda wa siku mbili baada ya kutoka kwenye ziara ya Kihistoria huko Vatican ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francis.

Picha: Ziara ya Rais Samia Nchini Norway

 

Namna bora ya kumuenzi Lowassa ni kuyaishi maono yake - Dkt. Mwinyi
Kambi ya upasuaji wa Moyo BMH yaanza