Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi umedhamiria kuwapa nafasi makampuni ya upangaji na upimaji yanayomilikiwa na Watanzania nchini katika utekelezaji wa mradi kwenye maeneo ya urasimishaji mijini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Upangaji na Upimaji kutoka Wizara ya Ardhi Bw. Mazula Manyasa alipofungua mafunzo kwa makampuni ya upangaji na upimaji tarehe 14 Februari 2024, Jijini Dodoma yaliyoandaliwa na Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi.
Amesema, utekelezaji wa kazi za mradi uko katika makundi mawili ambayo ni asilimia 20 inayoendelea kutekelezwa na watumishi wa Serikali pamoja na asilimia 80 ambayo inatarajiwa kutekelezwa na makampuni ya upangaji na upimaji yaliyopo nchini.
‘‘Wizara imeandaa mafunzo haya kwa makampuni ya upangaji na upimaji ili kujenga uelewa juu ya mradi na kazi mbalimbali zinazotegemea kufanyika ikiwa ni hatua muhimu kabla ya zoezi la manunuzi ambalo litalenga kuyashindanisha makampuni ya upangaji na upimaji na kupata makampuni yatakayoshiriki kazi za urasimishaji katika maeneo mbalimbali ya Mradi’’ alisema Manyasa.
Naye Meneja Urasimishaji kwa upande wa Mjini, Leons Mwenda alisema kuwa kusudi la mafunzo hayo ni kujenga uelewa wa pamoja juu ya kazi mbalimbali za mradi na masuala muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa mradi hasa masuala ya kimazingira na kijamii ili kuwa na mtazamo mmoja pamoja na wananchi katika utekelezaji wa mradi.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi ni mradi unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa muda wa miaka mitano (2022-2027) ikiwa na lengo la kuongeza usalama wa milki za ardhi.