Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika (EAPP Council of Ministers-COM) limekubaliana kwa pamoja kuwa na usimamizi madhubuti wa miradi mbalimbali ya umeme katika nchi wanachama, ili iweze kukamilika kwa wakati na kuwapatia wananchi nishati ya kutosha.

Kukamilika kwa miradi kutoka vyanzo mbalimbali vya umeme, kutawezesha nchi hizo kusaidiana pale nchi mojawapo inapokuwa na upungufu wa umeme huku msisitizo ukiwekwa kwenye miradi ya usafirishaji umeme.(Transmission lines).

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika
(EAPP Council of Ministers-COM) ambao unafanyika kwa siku mbili jijini Nairobi, Kenya.

Amesema, “Baraza hili ni muhimu katika kuhakikisha nchi za Afrika zinaungana kwa ajili ya kuendeleza rasilimali za umeme zilizopo pamoja na kupata umeme wa uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na katika Mkutano huu kila nchi imeonesha utayari kufanya biashara ya umeme pale kunapokuwa na umeme wa ziada.”

Dkt. Biteko meongeza kuwa, Tanzania itakuwa sehemu ya soko la umeme pale nchi jirani zitakapohitaji nishati hiyo, na hii ni baada ya kuwashwa kwa mashine zote Tisa katika Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo litazalisha megawati 2,115 ambazo zinatoa uhakika wa kutosheleza mahitaji ya ndani.

“Tanzania kuna njia mbalimbali za usafirishaji umeme (interconnectors) mfano Tanzania na Uganda, Tanzania na Burundi pamoja na Tanzania na Rwanda na sasa kuna laini ya umeme kutoka Tanzania hadi Kenya ambayo imekamilika na ipo kwenye majaribio itakayotuwezesha kufanya biashara kati ya nchi hizi mbili pale kila nchi ikiwa na umeme wa kutosha.”amesema Dkt. Biteko.

Aidha, amesisitiza kuwa nchi Wanachama zinapaswa kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili kupunguza changamoto za umeme kwani umeme huo utaweza kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine na kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika

Awali, Mwenyekiti wa kikao hicho cha Baraza la Mawaziri wa Nishati ambaye ni Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, Mhe. Davis Chirchir amesema lengo la nchi kuwa na mfumo huo ni nchi wanachama 13 kufanya biashara ya mauziano ya umeme pale kunapokuwa na ziada ya umeme, na kwamba ili suala hilo liwezekane lazima kuwepo na miumbombinu ya umeme inayounganisha nchi hizo.

Amesema kuwa, majadiliano ya viongozi hao yamelenga katika kuimarisha muundo wa umoja huo pamoja na ushirikiano na hii ikijumuisha namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za umeme pale zinapojitokeza.

Ameongeza kuwa, takriban watu milioni 600 bado hawajapata nishati ya umeme barani Afrika kati ya watu takriban Bilioni 1.5 na hii ikionesha jinsi nguvu zaidi inavyohitajika ili kuwa na nishati ya kutosha kuweza kukidhi mahitaji.

Nchi Wanachama wa Umoja wa EAPP ni pamoja na Kenya, Tanzania, Sudan Kusini, Sudan, Uganda, Somalia, Libya, Ethiopia, Misri, Djibouti, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo kikao hicho kimehudhuriwa na Wadau wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).

Viongozi wengine wanaoshiriki Mkutano huo kutoka Tanzania ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima-Nyamohanga.

Tanzania ina nafasi kuwa kitovu cha Madini Afrika - TGJTA
Simba SC, Young Africans wapewa waamuzi wa AFCON