Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amezitaka Halmashauri ikiwemo ya Wilaya ya Kilwa kuajiri watumishi wa mikataba kwa kutumia mapato ya ndani, ili kupunguza changamoto za uhaba wa wataalamu wa Afya katika Wilaya hizo.

Waziri Ummy ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya hali ya Afya katika Halmashauri ya Wilaya hiyo iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Lusajo Mwakajoka ambayo inaonyesha hali ya upatikanaji wa huduma za Afya katika Mkoa wa Lindi, upatikanaji wa Vifaa na Vifaa Tiba pamoja na changamoto.

Amesema, “tutatumia njia kuu Tatu ili kupunguza changamoto za watumishi ikiwa ni pamoja na njia ya vibali vya ajira kutoka Ofisi ya Rais Utumishi, kuajiri watumishi kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na wadau wetu wa maendeleo katika Sekta ya Afya nao wanaajiri ajira za mikataba pamoja.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amemshukuru Waziri wa Afya Mhe. Ummy kwa kufanya ziara katika Mkoa huo na kumuomba aupe kipaumbele kwa kuwa una wananchi wengi wa kipato cha chini ambao hushidwa kufata huduma mbali na makazi yao.

“Vifaa tiba ikiwemo Dawa zinaposambazwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) tunaomba wawe wanawahi kwa wakati kwa kuwa wananchi wengi wa Mkoa wa Lindi wanakipato cha chini, dawa zinapochelewa tunamkwamisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwakuwa ameshatoa fedha za dawa, kikubwa ni sisi watendaji.” Amesema Telack

Waziri Ummy anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Lindi na anatarajia kutembelea na kukagua hali ya utoaji wa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi (Sokoine), Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya pamoja na Zahanati.

Katika ziara hiyo Waziri Ummy aliambatana na timu kutoka Wizara ya Afya akiwemo Mkurugenzi Msaidizi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa Dkt. Caroline Damian anae muwakikisha Mkurugenzi wa huduma za Tiba, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali watu upande wa Hospitali za Rufaa za Mikoa, Danny Temba.

44 Wafariki kwa moto uliozuka Ghorofani
Makala: Falsafa ya Mzee Mwinyi na Demokrasia ya dirisha wazi