Lydia Mollel – Morogoro.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, imemhukumu miaka 25 jela John Mwaseba Mwasikili baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Bangi, zenye ujazo wa kilo 107.29.

Akitoa hukumu hiyo, Jaji wa mahakama M. P. Otaru amesema ushahidi uliotolewa na mashahidi 16 na vielelezo 15 vya upande wa mashitaka haukuacha shaka dhidi ya mshitakiwa kutenda kosa hilo.

Amesema, amemtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kujiridhisha kuwa ni kweli mshitakiwa alikamatwa na dawa ya kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilogram 107.29 iliyokuwa ndani ya gari aina ya Toyota Kluger namba T.895 CQR kwenye mifuko nane ya sulphate.

Mahakama pia imeamuru gari namba T 895 CQR ambalo lilikuwa na Bangi hiyo litaifishwe na kielelezo ambacho ni dawa za kulevya aina ya bangi kuteketezwa.

Mshitakiwa Mwasikili alikamatwa na Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya na kufikisha katika Mahakama kuu kanda ya Morogoro Machi 15, 2024.

Inadaiwa kuwa mwaka 2022 huko Morogoro lilikamatwa gari aina ya Toyota Kluger lenye namba za usajili T.985 ambalo ndani yake lilikutwa na mifuko nane ya sulphate ikiwa na dawa za kulevya aina ya bangi.

Mchengerwa: DART ipate mwekezaji binafsi
SUA yazitendea haki Bil. 73.6 za mradi wa HEET