Nahodha na Kiungo wa kikosi cha KMC FC, Awesu Awesu amesema watapambana kuhakikisha wanashinda mechi zao tisa zilizobaki ili kumaliza msimu ndani ya nafasi nne za juu.

Katika vita hiyo, KMC inapambana na timu za Coastal Union na Tanzania Prisons ambazo wanatofautiana kwa pointi mbili pekee.

Kiungo huyo ambaye yupo kwenye kiwango bora hivi sasa amesema lengo lao kubwa ni kushiriki michuano ya kimataifa kama ilivyokuwa misimu mitatu nyuma.

“Tumekuwa na msimu bora sana, itapendeza kama tutamaliza ndani ya nne bora ingawa najua vita ni kali, lakini tutapambana kwa ajili ya kutimiza lengo letu,” amesema Awesu.

Kiungo huyo ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ amesema mbali na kutaka kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao lakini anaamini timu hiyo itafanya usajili mkubwa zaidi, ili msimu ujao wawe miongoni mwa timu zinazowania ubingwa wa Ligi Kuu.

Amesema anajivunia ubora wa kikosi chao pamoja na uwezo mkubwa aliokuwa nao Kocha wao mkuu, Abdulhamid Moallin ambaye ameibadilisha timu hiyo kwa kiasi kikubwa.

KMC kwa sasa ipo nafasi ya sita kwenye msimamo ikiwa na pointi 28 na imezidiwa pointi mbili na Coastal Union waliopo nafasi ya nne na pointi zao 30.

Ibrahim Imoro anasakwa Msimbazi
Waandishi wawili wafariki kwa ajali Lindi