Siku mbili zikisalia kabla ya kushuka dimbani katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), takwimu za Mamelodi Sundowns ikiwa nyumbani katika mechi za Robo Fainali ya michuano hiyo, zinaipa Young Africans itachuana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini keshokutwa Ijumaa (Aprili 05) saa 3:00, Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria nchini Afrika Kusini.

Timu hiyo yenye maskani katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani itaingia katika nafasi mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza uliopigwa Jumamosi (Machi 30) katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Ili kutinga Nusu Fainali, Young Africans inahitaji ushindi au sare ya kuanzia bao 1-1 katika mechi ya marudiano.

Hata hivyo, rekodi za matokeo ya Mamelodi Sundowns katika mechi tano zilizopita za Robo Fainali ilizokuwa katika dimba la nyumbani, zinaipa nafasi Young Africans inayonolewa na Miguel Gamondi kufanya vyema kama itajipanga vizuri.

Kwa mujibu wa kuanzia msimu wa 2018/2019 hadi msimu uliopita, Mamelodi imecheza Robo Fainali ya CAFCL mara tano, huku ikishinda mechi mbili kati ya tano ilizokuwa katika dimba la nyumbani na kutoka sare mara tatu.

Iko hivi, msimu uliopita ambao timu hiyo iliishia Nusu Fainali, ilishinda mabao 2-1 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria katika mchezo wa nyumbani wa Robo Fainali wakati msimu wa 2021/2022 ikitoka sare ya bao 1-1 ilipocheza na Petro de Luanda ya Angola na kutolewa kwa matokeo ya jumla ya 3-1.

Timu hiyo maarufu kama Masandawana ilipangwa na Al Ahly ya Misri katika Robo Fainali ya mwaka 2020/21, ambapo katika mechi ya nyumbani ilitoka sare ya bao 1-1 na kutolewa kwa jumla ya mabao 3-1 kama ilivyotolewa katika msimu wa 2019/2020 na Wamisri hao ambapo katika mechi iliyopigwa Afrika Kusini timu hizo zilitoka sare ya 1-1.

Katika msimu wa 2018/2019, Mamelodi ilipata ushindi wa mabao 5-0 ikiwa nyumbani dhidi ya Al Ahly na kupenya hatua ya Nusu Fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1.

Mbali na takwimu hizo, makocha na wachambuzi wa soka nchini wameipa nafasi Young Africans kufanya vyema katika hatua hiyo na kutinga Nusu Fainali ya CAFCL msimu huu.

Kocha wa zamani wa Young Africans, Kenny Mwaisabula amesema timu hiyo kongwe nchini ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mechi ya marudiano kutokana na ubora wa kikosi na mbinu za Muargentina Gamondi.

“Endapo kikosi cha cha Young Africans kitakamilika bila kukosekana kwa wachezaji watatu ambao hawakuwepo katika mchezo uliopita, nina imani wakijituma watafuzu Nusu Fainali,” amesema Mwaisabula ambaye pia ni mchambuzi wa soka.

Kocha wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Maalim Salehe ameipa Young Africans nafasi kubwa ya kuitoa Mamelodi Sundowns katika mechi hiyo.

“Nina imani na uwezo wa walimu wa Young Africans, kwa sababu mchezo uliopita walitumika wachezaji wa akiba baada ya baadhi yao kupata majeraha lakini hawakufungwa,” amesema Salehe.

Hata hivyo, kocha huyo alikiri mchezo huo wa marudiano utakuwa mgumu kutokana na timu zote mbili kuwa na wachezaji bora.

Shughuli za Bandari zimeongezeka: Mrisho
Taasisi zinazochakata taarifa binafsi kuzingatia sheria